Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 14Article 551539

Habari za Mikoani of Saturday, 14 August 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwendo kasi, kuchomekea, uzembe chanzo ajali ya DC Msando

Mwendo kasi, kuchomekea, uzembe chanzo ajali ya DC Msando Mwendo kasi, kuchomekea, uzembe chanzo ajali ya DC Msando

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Furtunatus Muslim, amesema chanzo cha ajali ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msondo, ni mwendo kasi wa dereva aliyekuwa akimuendesha DC huyo ambaye pia alipita magari mengine ili kuwahi msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, uliyekuwa na ziara mkoani Morogoro.

Muslim, amesema kuwa awali Waziri Mkuu alitembelea Mashamba ya Mkulanzi na baadae kwenda kiwanda cha kuchakata nyama cha Mbigiri ambapo wakiwa njiani kuelekea kwenye kiwanda hicho ndipo walipata taarifa ya Msando kupata ajali.

Alisema gari lililokuwa limembeba Msando na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Ngolo Malenya lilichelewa msafara kitendo ambacho kilimfanya dereva wa gari hilo kuendesha kwa kasi na kuchomekea magari mengine lengo likiwa kuwahi msafara huo ambao uliwaacha mbali.

“Ajali imetokea katika eneo la Mkongeni Bwawa la hatari, ambapo gari la Mkuu wa Wilaya lenye namba STL 911 Toyota Landcruzer ambalo lilikuwa limembeba DC huyo na DC wa Ulanga, Ngolo Malenya, dereva 'aliovertake' ili awahi kuungana na msafara.

“Inavyoonekana wakati tunatoka Mkulanzi, gari la DC lilichelewa kutoka askari wa usalama barabarani wakaruhusu msafara kupita na baada ya magari yote ya msafara kupita, wakaruhusu magari mengine ya wananchi, ndipo gari la DC ambalo lilikuwa limeachwa nyuma zaidi na msafara dereva akawa kasi sana akachomekea magari mengine ili awahi.

“Kutokana na uharaka na kuchomekea magari mengine akagongana na gari la Wizara ya Afya Makao Mkuu Dodoma lenye namba DFP 8530 Toyota Land Cruzer ambalo baada ya kugongwa na gari ya DC lilirudi nyuma na kugonga gari namba T 131 DPC Toyota Illux lililokuwa limebeba raia wa kichina.” alisema Muslim

Alisema gari la DC Msando na lile la Wizara ya Afya yote yamepinda boneti wakati gari lililokuwa na raia wa kichina limebonyea ubavuni.

Alisema majeruhi wote wamekimbizwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro kwa matibabu.