Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 20Article 552661

Habari Kuu of Friday, 20 August 2021

Chanzo: globalpublishers.co.tz

Mwigulu: Tumekusanya Bil 48.4 za Tozo, Aibu Miradi ya JPM Kukwama

Mwigulu: Tumekusanya Bil 48.4 za Tozo, Aibu Miradi ya JPM Kukwama play videoMwigulu: Tumekusanya Bil 48.4 za Tozo, Aibu Miradi ya JPM Kukwama

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, tangu tozo za miamala ya simu kuanza tayari Tsh bilioni 48.4 zimepatikana huku Tsh bilioni 37 zikielekezwa kwenye ujenzi wa vituo vya afya kwa maeneo ambayo hayakuwahi kuwa na vituo hivyo na Tsh bilioni 7 zikienda kwenye ujenzi wa madarasa.

MDkt. Mwigulu amesema hayo leo Ijumaa, Agosti 20, 2021 wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam.

“Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, kitendo cha kuaminiwa na Bodi ya Benki ya Dunia (WB) na hata kupewa miradi mitano ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Tsh trilioni 2.6, ni kitendo kikubwa.

“Tunapaswa kutambua kuwa nchi ni yako mwananchi, fedha ni zako lakini pia tuliyoyapanga kuyafanya ni yetu pia. Hivi ndivyo inavyokuwa katika nchi inayojitawala. Niwashukuru wote waliolielewa kwa kiasi hicho. Kama serikali tutaendelea kupokea na kuyafanyia kazi maoni yote, na haijalishi mtoa maoni yuko Serikalini au la, kwetu maoni ni maoni muhimu maoni hao yanalenga kujenga nchi yetu.

“Tulikiri katika nchi yetu kuwa kuna miradi mikubwa ya kimkakati na tulikubaliana wote kuwa ni lazima iendelee, miradi hii ni ndoto yetu ambayo tunataka itimie. Kwetu sisi Watanzania walio hai kwa sasa itakuwa ni aibu kwetu kwamba, miradi ya kimkakati imekwama eti kwasababu aliyeianzisha miradi hiyo hayupo.

“Tangu makato ya tozo yaanze kwa hizi Wiki 4 hadi leo tumekusanya zaidi ya Tsh bilioni 48.4, zaidi ya Tsh bilioni 22 tulishapeleka kwenye maeneo ambayo hayana vituo vya afya (zaidi ya vituo 90), leo tumepeleka zaidi ya Tsh bilioni 15 kwenye eneo hilohilo na kufanya vituo kuwa zaidi ya 150, Tsh bilioni 7 zikienda kwenye ujenzi wa madarasa zaidi ya 500, ni watoto wetu wanasoma.“

“Kuanzia mwaka kesho tutaanza kupokea kidato cha tano ambao wametokana na sera ya elimu bila malipo, tunafahamu mahitaji yatakuwa ni makubwa. Tunaona kabisa mambo haya tunapaswa kuyafanyia kazi na si kuyaahirisha.

“Bado yapo maeneo nchini ili uweze kufika kwenye kituo cha afya inakulazimu uende ama kwenye kata nyingine au tarafa nyingine, kwa umuhimu wa jambo hili tukasema sio la kuacha bila kufanyia kazi.

“Hapa katikati kuliibuka maneno mengi sana na ilielezwa kwamba shughuli za miala ilipungua, niseme kwamba Watanzania waliendelea kutumiana na shughuli za kufanya miamala hazikuathirika na takwimu ziko pale pale, ni kati ya Tsh milioni 9 hadi Tsh milioni 11.

“Sisi Wizara ya Fedha na Mipango tunaamini kwamba, tunapopeleka Bil 48 kwenye uchumi maana yake tunaongeza kasi ya kutumiana fedha na kuifanya fedha iende kwenye mzunguko na kasi ya kubadilisha fedha kwenye mikono itaongezeka pia.

“Katika suala la tozo za miamala ya simu kwa sasa, kuna gharama za mtoa huduma na gharama zilizowekwa na serikali, lakini jumla yake yote anabeba mwananchi.

“Tukaangalia hili suala la tozo za miamala ya simu, tukasema hakuna namna ya kwamba serikali na watoa huduma tukae kwa pamoja tuone namna gani tutampunguzia gharama ya jumla kwa mwananchi. Tupo katika hatua ya mwisho katika hili.

“Suala la kusubiri hata matundu ya vyoo nchi fulani ije kutujengea si jambo zuri na haituletei heshima na wakati huo sisi tupo, niwaombe Watanzania hizi shughuli zetu, tuendelee kushikamana,” amesema Mwigulu.