Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 585007

Habari za Mikoani of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Mwili wa Rubani Mazula waagwa Dar

Mwili wa Rubani Mazula Aagwa Dar Mwili wa Rubani Mazula Aagwa Dar

Mwili wa rubani mstaafu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Kapteni Deogratius Mazula (77), umeagwa jana katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi Sinza mkoani Dar es Salaam na utazikwa leo katika makaburi ya Njiro –Arusha.

Idadi kubwa ya ndugu, jamaa na marafiki imejitokeza kanisani hapo kuuaga mwili wa rubani huyo aliyehudumu ATC wakati huo sasa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), akiwa kati ya Watanzania wa mwanzo kurusha ndege za ATC.

Katika mahubiri yake, Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mwokozi, Padri Cuthbert Maganga alibainisha kuwa Kapteni Mazula aliamini Mungu kila wakati kiasi cha kuomba hata kufanyiwa ibada nyumbani.

“Huyu alikuwa ana imani kwa Mungu na alimkabidhi maisha yake na ilifikia hatua hasa kutokana na ugonjwa wake alikuwa akipatiwa huduma za kiroho nyumbani kwake, hakina amepokelewa mahala pema peponi, na tuliobaki tunapaswa kuendelea kuishi maisha yanayompendeza Mungu,” alisema Padri Maganga.

Akizungumzia sababu ya kifo cha Mazula, mtoto wake Joyce Mazula alisema Kapteni Mazula alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya tangu mwaka 2003 hasa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la mifupa ya mgongo iliyosababisha kufanyiwa upasuaji mara kadhaa nchini India na hapa nchini.

Ilipofika Januari 6, mwaka huu hali yake ilibadilika ghafla na katika harakati za kumpeleka hospitali, aliaga dunia.

Akizungumzia historia yake, alisema Kapteni Mazula alizaliwa Septemba 15, 1944 na alisoma elimu 

ya awali katika Shule ya Busongo mkoani Tabora na sekondari alisoma Pugu Sekondari wakati huo ikiitwa Saint Francis.

Baada ya hapo, alijiunga na kidato cha tano na sita katika Shule ya Mtakatifu Marko and Georges ambayo kwa sasa ni Mkwawa iliyopo Iringa kati ya mwaka 1964 hadi 1965 kisha baada ya kumaliza mwaka huo alijiunga na mafunzo ya urubani hadi 1967 ambako alisomea Chuo cha Oxford Air Training School kilichopo Uingereza.

Akizungumzia historia yake, Joyce alisema Kapteni Mazula alipomaliza masomo aliajiriwa Wizara ya Mawasiliano kisha kuhamia Shirika la Ndege la Afrika Mashariki kabla ya kwenda kufanya kazi Williamson Diamonds Limited.

Alisema katika ofisi zote alikuwa akihudumu kama rubani wa ndege, na pia aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Ndege la Msumbiji na baadaye Shirika la Ndege la Kenya kabla ya kurejea Tanzania na kuhudumu ATC.

Kapteni Mazula atakumbukwa kutokana na kuwa rubani wakati wa tukio la utekaji ndege ya ATC mwaka 1982 aina ya Boeing 733 lililofanywa na vijana wanne wa Kitanzania wakishinikiza kujiuzulu kwa Rais Julius Nyerere.

Ndege hiyo ilikuwa ikitokea Mwanza kwenda Dar es sakaam, lakini iliamuriwa na watekaji kupelekwa Nairobi na kisha Jeddah, Saudia Arabia, Athens Ugiriki kabla ya kutua Uingereza ambako vijana hao walipewa hifadhi ya ukimbizi.

Alisema alifunga ndoa na mkewe Ramla Nkya ambaye ameshatangulia mbele ya haki na wameacha watoto sita, wawili wa kiume na wanne wa kike. Ameacha wajukuu watano na kitukuu mmoja. Mwili huo ulisafirishwa jana kwa ATCL.