Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 541018

xxxxxxxxxxx of Friday, 4 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwili wa mwalimu aliyeuawa kwa kisu kuagwa leo

MWILI wa Mwalimu wa Shule ya Msingi Segerea, jijini Dar es Salaam, Flora Mariki (37), aliyefariki dunia akidaiwa kuchomwa na kitu chenye ncha, unaagwa leo na utasafirishwa kupelekwa Rombo, Kilimanjaro kwa maziko.

Mtoto wa shemeji ya Flora anadaiwa kumuua mwalimu huyo kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Janeth Magomi jana alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Eufrasia Ibrahimu Assenga (21).

Kamanda Magomi alilieleza HabariLEO kuwa mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi wa tukio hilo unaendelea na kwamba polisi wameruhusu mwili utolewe hospitali kwa ajili ya maziko.

Juzi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema mauaji hayo yalifanywa Jumapili usiku wa kuamkia Juni Mosi na yalitokana na ugomvi wa kifamilia.

“Tuna tukio la mauaji linalodaiwa kutokana na ugomvi wa kifamilia, tunaendelea na upelelezi, tunamshikilia kituo cha Polisi Stakishari, Eufrasia Ibrahim Assenga, binti ambaye anadaiwa kumchoma na kitu chenye ncha kali marehemu Flora ambaye ni mama yake mdogo na kufikwa na umauti,” alisema Kamishna Janeth.

Majirani wa marehemu Flora ambaye ni mkazi wa Ukonga Stakishari, jijini Dar es Salaam ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walidai juzi kuwa kwa muda mrefu Flora alikuwa akilalamika kuwa Eufrasia hampendi licha ya kumlea kama mama yake.

Walidai kuwa tangu akiwa darasa la nne Eufrasia au jina la nyumbani ‘kamamaa’ alilelewa na familia ya Kasmiri Assenga ambaye ni baba yake mdogo na mume wa marehemu.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio Flora na mumewe, Kasmiri Assenga walikuwa wakizungumza na binti huyo masuala ya shule na ndipo kukatokea sintofahamu baina ya Flora na msichana huyo lakini Assenga alisuluhisha.

Inadaiwa baada ya hapo Assenga aliingia chumbani na kisha Flora alifunga mlango na kumwambia mumewe ngoja amfundishe adabu msichana huyo.

Inadaiwa katika ugomvi huo mama huyo alichomwa kisu maeneo mbalimbali ya mwili.

Inadaiwa Flora aliishiwa nguvu na kudondoka kisha binti huyo akaenda kufungua mlango wa chumbani na ndipo mume wa mama huyo alitoka na kwenda alipokuwa mkewe akajaribu kumfunga majeraha damu isiendelee kutoka.

Taarifa zinadai baada ya hapo mume wa Flora akiwa na mtuhumiwa walimchukua mama huyo na kumkimbiza zahanati binafsi ya jirani iitwayo Decent akapata tiba ya awali na walitakiwa wampeleke mgonjwa Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini wakiwa njiani alifariki dunia.

Inadaiwa kuwa, Polisi walipewa taarifa kuhusu kifo hicho na ndipo mtuhumiwa alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Stakishari.

HabariLEO jana ilifika nyumbani kwa marehemu Ukonga Stakishari ambapo mume wa marehemu, Kasmiri Assenga alisema leo mwili wa marehemu utaletwa nyumbani na mchana utapelekwa Kanisa Katoliki la Stakishari kwa ajili ya ibada ya mazishi.

Baada ya ibada na shughuli za kuaga kumalizika mwili utasafirishwa jioni kupelekwa Mahiwa, Mamsera, Rombo mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko Jumamosi.

Join our Newsletter