Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541879

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mzindakaya kuzikwa Ijumaa Sumbawanga

Mzindakaya kuzikwa Ijumaa Sumbawanga Mzindakaya kuzikwa Ijumaa Sumbawanga

MWANASIASA mkongwe na mfanyabiashara, Dk Chrisant Mzindakaya (80) anatarajiwa kuzikwa Ijumaa mkoani Rukwa.

Mtoto wa Mzindakaya, Jacqueline Mzindakaya alilieleza HabariLEO kuwa mwili wa marehemu utaagwa Dar es Salaam na nyumbani kwake Sumbawanga.

Jaqueline alisema mwili wa mzee Mzindakaya utatolewa hospitali ya Taifa Muhimbili leo asubuhi na kupelekwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro, Oysterbay kwa ajili ya misa Takatifu na kumuaga.

"Baada ya hapo msafara utaelekea kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere kwa ajili ya safari ya kuelekea mjini Sumbawanga katika makazi ya mzee wetu katika kipindi chote cha maisha yake na ndiko alikosisitiza kuwa akifariki azikwe nyumbani kwake," alisema.

Jaqueline alisema kesho waombolezaji watapata fursa ya kuaga hadi siku ya maziko Ijumaa.

Mzee Mzindakaya alishika nyadhifa serikalini kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza hadi Serikali ya Awamu ya Tano.

Wakati wa awamu ya kwanza aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkuu wa Mkoa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Kigoma na Rukwa na baadaye kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) hadi alipostaafu wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Jacqueline alisema baada ya mzee Mzindakaya kustaafu shughuli za serikali alirudi Sumbawanga na kujishughulisha na miradi hasa ufugaji.

Kwa mujibu wa familia ya marehemu, mzee Mzindakaya alianza kusumbuliwa na mrija wa kusafirisha nyongo kwamba uliziba hivyo akapelekwa katika hospitali ya Aga Khan Aprili mwaka huu akafanyiwa upasuaji.

Baadaye alihamishiwa Muhimbili ambako alifanyiwa upasuaji mwingine mara nne na aliendelea na matibabu hadi Juni 7 alipoaga dunia. Dk Mzindakaya alizaliwa Desemba 31, 1940 mkoani Rukwa.

Alijiunga na Shule ya Sekondari Bugerere nchini Uganda katika ya 1960-1961, mwaka 1963-1964 alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Jamii,Tengeru mkoani Arusha kwa ngazi ya cheti.

Katika miaka ya 1964 na 1965 alikuwa Ofisa Maendeleo Msaidizi Wilaya ya Sumbawanga. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Biashara ya Ndani (BIT) katika miaka ya 1973-1975.

Mwaka 1975- 1987 alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Viwanda Vidogo nchini (SIDO), 1969-175 alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Tanu" TANU Youth League).

Mwaka 1992 alikwenda masomoni Dublin nchini Ireland kusomea mafunzo ya utawala na mipango ya maendeleo kwa ngazi ya cheti.

Mwaka 1990- 1992 alikuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Rukwa, mwaka 1990- 1997 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapipunduzi (CCM).

Wakati huohuo CCM kimesema kimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Dk Mzindakaya.

Taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ilieleza kuwa Dk Mzindakaya alikuwa kiongozi mwandamizi katika chama hicho na serikali tangu wakati wa TANU na baadaye CCM.

Shaka alitaja miongoni mwa nyadhifa alizoshika mzee Mzindakaya kuwa ni Katibu wa CCM wa Mkoa, Mbunge, Mkuu wa Mkoa kwenye mikoa tofauti na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.

"Chama Cha Mapinduzi kimempoteza kiongozi mahiri, mchapakazi, mzalendo na mwenye msimamo usiyoyumba katika kupigania maslahi ya taifa wakati wote wa utumishi wake ndani ya chama na serikali na hata baada ya kustaafu alikuwa na mchango mkubwa katika kutika ushauri kulisaidia taifa" alisema.

Join our Newsletter