Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 26Article 539875

Habari Kuu of Wednesday, 26 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCAA yamtii Samia, yahama hifadhini

NCAA yamtii Samia, yahama hifadhini NCAA yamtii Samia, yahama hifadhini

KATIKA kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kupunguza shughuli za kibinadamu ambazo zimekuwa na athari kubwa kwenye eneo la Ngorongoro, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imesema mpaka ifikapo mwisho wa mwezi huu itakuwa imehamisha Makao Makuu yake kutoka ndani ya hifadhi hiyo kwenda Karatu.

Wakati akiwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu Aprili 7, mwaka huu Ikulu Dar es Salaam, Rais Samia alisema Ngorongoro inapotea kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.

Rais Samia alisema Ngorongoro ni eneo la aina yake na licha ya kwamba yalifanyika makubaliano ya watu na wanyama wakae pamoja, lakini kwa sasa idadi ya watu imezidi zaidi kuliko wanyama.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCCA, Dk

Freddy Manongi, sababu ya kwanza ya kuhamisha Makao Makuu hayo ni kupunguza shughuli za kibinadamu ambazo zimekuwa na athari kubwa kwenye eneo la Ngorongoro.

Aliitaja sababu ya pili ya kuhamia mjini Karatu kutoka hifadhini kuwa ni ukubwa wa gharama za uendeshaji.

Alisema gharama za kuendesha shughuli zao kutokea ndani ya hifadhi ni kubwa na zinapungua zaidi wakifanya shughuli hizo nje ya hifadhi.

“Tuliagizwa na serikali na Bodi ya Wakurugenzi ambayo ndiyo inatuongoza na wizara kwa ujumla kuhusu eneo la Makao Makuu ya Ngorongoro. Kwa hiyo leo (jana) ningependa kuwataarifu kwamba tumeamua kufanya maamuzi rasmi ambayo ni maagizo ya kuhama kwa kuyatoa Makao Makuu kutoka Ngorongoro kuyapeleka Karatu,” alisema Dk Manongi alipotangaza hatua hiyo hivi karibuni.

Aliongeza “Kwa hiyo tumeona ili kupunguza shu-

ghuli za kibinadamu na uonekano wa binadamu ndani ya hifadhi, ni vizuri tutekeleze maagizo haya ambayo tumepewa na tunahamia rasmi Karatu na mwisho wa mwezi huu tutakamilisha kazi ya kuhamia Karatu.”

Dk Manongi alisema hivi karibuni yametokea mabadiliko ambapo serikali imewaagiza kuwa shughuli zote za jamii zitekelezwe na halmashauri jambo ambalo lipunguza shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi na kuzipeleka nje.

“Pia tuna taratibu na sheria nyingi zinazotuongoza katika kufanya shughuli zetu. Ukiangalia miongozo inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) na Shirika la Kimataifa la Kutetea Uhifadhi (IUCN), inataka makao makuu ya hizi hifadhi yawepo nje ya maeneo ya uhifadhi,” alisema Dk Manongi.

Alisema kutokana na miongozo hiyo ya Unesco na IUCN, kuna haja ya kuitii

miongozo hiyo na kuchukua mwelekeo wa kupunguza shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi na kwenda nje ya hifadhi.

Alipozungumza Ikulu, Rais Samia alisema, “Tulipoingia kwenye huu mkataba tulikuwa na idadi ya watu 9,000 Ngorongoro, sasa wako watu 90,000 hadi 100,000, lakini mamlaka na wizara mpo mnaangalia tu maeneo ya Ngorongoro yanachukuliwa. Watu 100,000 ni wengi, wanyama watazidiwa tu.”

Pia alisema Ngorongoro inatoweka kutokana na uvamizi wa viumbe vigeni ikiwemo miti na vidudu na kufanya wanyama wapande juu na kutoweka katika eneo hilo.

Tayari NCAA imeanza kuondoa viumbe vamizi kwani hivi karibuni Dk Manongi aliwaongoza watumishi wa mamlaka hiyo kufanya operesheni maalumu ya kufyeka mimea vamizi ambayo imeathiri maeneo mbalimbali ya eneo la hifadhi.

Katika operesheni hiyo, Dk Manongi anasema mimea vamizi ya aina mbalimbali imeathiri maeneo ya ndani ya hifadhi hususan maeneo ya Ndutu, Olduvai na eneo la Kreta ya Ngorongoro ambalo takribani hekta 5,000 sawa na asilimia 22 ya eneo lote la kreta, limeathiriwa na mimea hiyo.

Dk Manongi anasema pamoja na kazi hiyo kuwa imekuwa ikifanyika miaka yote, bado mimea hiyo imekuwa ikiongezeka kutokana na kuwapo kwa mvua nyingi hasa za mwaka jana (2020).

Katika hotuba yake Ikulu, Rais Samia alisisitiza kuwa endapo bado kuna haja ya kutaka Ngorongoro ibakie na iendelee kuitangaza Tanzania, hakuna budi kuongeza umakini wa kuitunza na kuhakikisha inabaki kwenye hadhi yake.

“Lakini jambo la kushangaza ni kwamba wafanyakazi wa Ngorongoro nao wanakata maeneo, wanajenga na kuhamia humo ndani. Wanastaafu na wanahamia

humo ndani na tunawaangalia tu wakati tunajua hili ni eneo la hifadhi. Kwa hiyo ama tukaiokoe au kama tunaamua kama Watanzania kwamba Ngorongoro kwa heri, basi tuseme kwa dunia kwamba Ngorongoro kwaheri tufuteni huko kwenye urithi wa dunia,” alisema Rais Samia.

Februari mwaka jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, Profesa Abiudi Kaswamila alinukuliwa na vyombo vya habari akisema wakati hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 kulikuwa na mifugo 200,000 lakini kwa sasa kuna mifugo zaidi ya 800,000 wakati ukubwa wa eneo ni uleule wa kilometa za mraba 8,292.

Miongoni mwa shughuli za kibinadamu zinazofanywa kwenye hifadhi hiyo ni pamoja na kilimo, elimu, ujenzi wa makazi, uharibifu wa mazingira kutokana na ongezeko la watu na mifugo na uwepo wa viumbe vamizi.

Join our Newsletter