Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540703

xxxxxxxxxxx of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

NCMC wajiandaa upotevu wa misitu

KITUO cha Kitaifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kinafanya mchakato utakaowezesha kutolewa kwa taarifa mpya ya upotevu wa misitu nchini kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Kituo hicho kipo mkoani Morogoro katika eneo la Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na kinawajibika kutafiti na kupata takwimu za misitu nchini sambamba na utekelezwaji wa Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa.

Akizungumza na waandishi wa habari kutoka Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira (JET) hivi karibuni, Mkurugenzi wa NCMC, Profesa Eliakim Zahabu, alisema uharibifu wa mazingira uliopo sasa ni mkubwa.

Alisema endapo juhudi makini kulinda mazingira hazitozingatiwa, siku zijazo hazitokuwa nzuri kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 5.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2002 hadi 2013 kwa Tanzania Bara, ramani ya upotevu wa misitu nchini inaonesha hekta 469,420 hupotea kwa mwaka na kwa Zanzibar katika kipindi cha mwaka 2004 hadi 2012, hekta 3, 149 zimepotea.

Alisema baadhi ya mikoa inaonesha namna uharibifu wa misitu ulivyofanyika kwa kiwango kikubwa ikiwemo mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Tanga.

Alisema ipo haja ya kuwepo kwa nguvu ya ziada ya kutunza mazingira na kupanda miti kwa wingi.

“Kwa mfano, Mkoa wa Kigoma uharibifu wa misitu unaelezwa kufanywa na wakimbizi wakikata miti kwa ajili ya kufungua mashamba kwa kiwango kikubwa, lakini kwa Mkoa wa Tabora kilimo cha tumbaku kimekuwa kikiathiri mazingira,” alisema.

Mkuu wa Ndaki ya Wanyamapori, Misitu na Utalii wa Sua, Profesa Suzana Augustino, alisema Tanzania ni nchi mwanachama wa Mpango wa Kudhibiti Mabadiliko ya Hali ya Hewa unaolenga kupunguza gesijoto ambayo kwa namna moja hadi nyingine imekuwa na athari mbalimbali.

Alisema miongoni mwa athari za gesijoto ni pamoja na kuongezeka kwa ukame, kuwepo kwa mafuriko ya mara kwa mara na hata kutoweka kwa visiwa vidogo na bayoanui mbalimbali.

Join our Newsletter