Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 20Article 558463

Habari Kuu of Monday, 20 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

NEMC, viongozi wa dini kujadili kelele

NEMC, viongozi wa dini kujadili kelele NEMC, viongozi wa dini kujadili kelele

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limepanga kukutana na viongozi wa dini na wenye baa na kumbi za starehe ili kuja na makubaliano ya kudhibiti tatizo la kelele na mitetemo katika maeneo ya makazi.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk Samweli Gwamaka alisema hayo wakati akizungumza na HabariLEO kwa njia ya simu.

Alisema kama Baraza wamejitahidi kadri ya uwezo wao kushughulikia tatizo hilo na bado wanaendelea kuchukua hatua stahiki kukabiliana nalo.

Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa Septemba 27 mwaka huu wanatarajia kukutana na viongozi wa dini na tayari wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo.

Alisema Septemba 30 mwaka huu, NEMC imepanga kukutana na wamiliki wa baa na kumbi za starehe.

“Wote hawa tutakutana nao kwenye semina juu ya athari za afya za kelele na mitetemo iliyopita kiwango katika maeneo ya makazi. Semina hizi zitahudhuriwa na watendaji mbalimbali wanaohusika na udhibiti wa mitetemo hii, vikiwemo vyombo vya dola,” alisema na kuongeza;

“Unajua mchawi mpe mwanao akulele sasa tunataka tukutane nao ili tujadiliane na kuelimishana na kisha tuje na makubaliano ya pamoja ili kila mmoja akayatekeleze na kumaliza kabisa tatizo hili,”

Juni 29 mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Selemani Jafo aliagiza wamiliki wa kumbi za starehe na burudani kuhakikisha sauti zitokanazo na shughuli zao hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria.

Alikuwa akitoa tamko kwa umma kuhusu udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo.

Alisema yeyote atakayesababisha kero zitokanazo na kelele na mitetemo kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa kelele na mitetemo) za mwaka 2015, atakuwa amevunja sheria na adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, sambamba na kufungiwa kwa biashara husika.

Pia, alitoa rai kwa viongozi wa dini kupitia Kamati za Amani, kulijadili suala hilo la kelele na mitetemo kutoka baadhi ya nyumba za ibada ili kupata namna bora ya kuziendesha kwa maslahi ya afya ya jamii.