Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 584884

Habari Kuu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

NEMC yaanza msako mkali dhidi ya wavunja sheria mifuko ya plastiki

NEMC yaanza msako mkali dhidi ya wavunja sheria mifuko ya plastiki NEMC yaanza msako mkali dhidi ya wavunja sheria mifuko ya plastiki

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) jana lilizindua rasmi msako wa wafanyabiashara wanaouza mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku mwaka 2019 kwa kuchafua mazingira ikiwemo vyanzo vya maji. Haya yanajiri baada ya bidhaa hizo haramu kuanza kuonekana katika masoko mbalimbali nchini, jambo ambalo kwa mujibu wa Nemc linaweza kurudisha taifa huko lilipotoka kabla ya Juni 2019 ilipopigwa marufuku kwa lengo la kupunguza uchafuzi wa mazingira. Ijumaa Nemc ilifanya ziara ya kushtukiza katika soko la Kisutu ambapo watu wawili walibainika kuwa na akiba ya mifuko iliyopigwa marufuku wakiendelea kuiuza kwa wauzaji wa reja reja wanaoiuza kwa watumiaji wa mwisho hivyo kuishia kwenye mazingira au vyanzo vya maji. Baada ya soko la Kisutu, msafara wa Nemc uliyofuatana na polisi ulivamia soko la Machinga Complex ambapo walikutana na katoni kubwa za mifuko ya plastiki iliyopigwa marufuku. “Tumeanza kazi ya kuwakamata kwa kukiuka sheria na bidhaa haramu wanazouza, leo tumekamata katoni zaidi ya 100 kwenye maduka yasiyozidi matano katika masoko mawili hapa Dar es Salaam lakini zoezi hili ni endelevu na litaendelea nchi nzima,” alisema mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Mazingira wa Nemc, Redempta Samwel. Alieleza kuwa wale wote ambao mizigo yao ilikamatwa itabidi waende ofisi za halmashauri siku ya Jumatatu (kesho) kwa ajili ya kuhojiwa kwa lengo la kuwapata wasambazaji wakuu ili wote waweze kuchukuliwa hatua za kisheria. “Kuna baadhi ya pakiti au katoni hazina nembo ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na nyingine zinaonyesha zimeagizwa kutoka nje ya nchi lakini ni feki licha ya kuwepo kwa mihuri hewa, watahojiwa na kutusaidie kutafuta viwanda vinazozalisha mifuko iliyopigwa marufuku nchini,” aliongeza Bi Samwel. Hata hivyo baadhi ya wafanyabiashara bidhaa zao zilizokamatwa wamesema hawana utaalamu wa kujua ni mifuko ipi halali na haramu kwa kuwa tayari mifuko hiyo ina mihuri ya mtengenezaji. “Tutajuaje? Bado hatuna ujuzi huu,” alilalamika Baraka Joseph, ambaye bidhaa zake zilichukuliwa. “Wafuate wazalishaji ambao ndio wanatuletea shida, maana tungekuwa tunafahamu tusingeweza kuuza kwa uwazi.” Baraza limepiga marufuku utengenezaji na uagizaji wa mifuko ya plastiki, hivyo mtu yeyote atakayekamatwa na kosa hilo atatozwa faini isiyopungua Sh20 milioni hadi Sh1 bilioni au kifungo cha miaka 2 au vyote kwa pamoja. Sheria hii haukuweza kumsahau hata msambazaji, mtu anayepatikana na hatia ya kosa hili, hutozwa faini isiyopungua Sh5 hadi Sh50 milioni- au kifungo cha miaka 2 au vyote kwa pamoja. Kwa muuzaji wa mifuko hiyo ya plastiki, atatozwa faini isiyopungua Sh100, 000 hadi Sh500, 000- au kifungo cha miezi 3 au adhabu zote mbili kwa pamoja. Na kwa mtu wa mwisho ambaye ni mlaji, akipatikana na hatia ya kosa hili, atatozwa faini isiyopungua Sh30, 000- au kifungo cha siku 7 au adhabu zote mbili kwa pamoja. Marufuku ya Usimamizi wa Kanuni za Mifuko ya Plastiki. Nambari 394 ya majukumu ya vikwazo ya 2019 yatatekelezwa na mtumiaji, mtengenezaji, msafirishaji, muagizaji na muuzaji wa mifuko ya plastiki