Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 27Article 540073

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

NHC kupangisha 80% ya nyumba mpya

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) linajipanga kutekeleza lengo la kuwapatia wananchi makazi bora kwa kutanua wigo wa uwekezaji.

Akiwasilisha bungeni Bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema ili kufikia lengo hilo katika mkakati wake wa muda mrefu, NHC inatarajia kubadili malengo ya nyumba mpya zitakazojengwa kutoka kuwa za kuuza asilimia 70 na kupangisha asilimia 30 na kuwa za kuuza asilimia 20 na kupangisha asilimia 80.

Lukuvi alisema pia kuanzia mwaka wa fedha 2021/2022 NHC itawekeza katika viwanda vya utengenezaji wa vifaa vya ujenzi vikiwemo vya kokoto, matofali na mabati

ili kuwapunguzia wananchi gharama za ujenzi wa nyumba.

Alisema katika muda wa kati, NHC inalenga kumalizia miradi mikubwa am-bayo imekwama na kuimarisha njia mbadala za mapato ili kuongeza kasi ya ukuaji wa shirika.

Alitaja mikakati hiyo kuwa ni kumalizia miradi mikubwa ambayo imekwama ikiwemo Morocco Square, Kawe 711, Golden Premier Residence na Mradi wa Kiwanja Namba 300 Regent Estate katika Jiji la Dar es Salaam.

“Ujenzi wa Morocco Square unaendelea kuanzia Novemba 2020 baada ya kusimama kwa muda. Hadi kufikia Mei 15, 2021, ujenzi umekamilika kwa 90%,” alisema Lukuvi.

Aliongeza, “Ujenzi wa Kawe 711, Golden Premier Residence na Mradi wa Kiwanja Namba 300 Regent Estate umesimama kwa muda, wakati jitihada za kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali zinaendelea. Kwa mwaka

wa fedha 2021/22 shirika limepanga kukamilisha Mradi wa Morocco Square.”

Lukuvi alisema mkakati mwingine ni kupitia upya mikataba ya wapangaji na kufan-ya maboresho ya vipengele ili kuhakikisha NHC inakusanya kodi na madeni.

Alisema NHC pia itakagua hali ya majengo yote ya shirika ili kuweka mpango wa kuzifanyia maboresho na matengenezo ya kudumu nyumba zake ili kuziongezea thamani.

“Hadi kufikia Mei 15, 2021, shirika limekamilisha mpango wa ukarabati uta-kaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2025/26 wenye lengo la kuboresha nyumba za shirika,” alisema.

Aliongeza, “Majaribio ya mpango huu yalifanyika katika mradi wa Medeli jijini Dodoma am-bapo nyumba zote zinazomilikiwa na shirika zimekarabatiwa.”

Alisema utekelezaji wa mpango huo unaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam (Temeke), Kilimanjaro na Mtwara.

Alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, NHC itaendelea kukarabati na kufanya matengenezo ya nyumba katika mikoa nchini na pia wizara kupitia shirika hilo ilitekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika halmashauri za miji na wilaya.

“Hadi kufikia Mei 15, 2021 shirika liliendelea na ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri za Miji,” alisema Lukuvi na kuongeza kuwa NHC pia litaanzisha miradi mipya ya nyumba za gharama nafuu katika halmashauri za Sumbawanga na Ubungo (Luguruni) na kuendelea kutekeleza miradi ya uendelezaji miji ya pembezoni katika maeneo inayoyamiliki ambayo ni Luguruni - Ubungo, Uvumba - Kigamboni na

Kawe - Kinondoni, Burka/ MatevesiArusha Jiji na eneo la Usa River - Meru.

Alisema pia NHC itaendelea na ujenzi wa majengo ya biashara katika halmashauri za manispaa za Lindi na Bukoba na kuanza ujenzi wa majengo ya biashara katika halmashauri za manispaa za Kahama na Morogoro na halmashauri za Wilaya za Masasi na Kilwa.

“Sambamba na utekelezaji wa miradi hiyo, shirika litafanya upembuzi yakinifu wa miradi ya ujenzi wa makazi na biashara katika mikoa ya Songwe, Ruvuma, Njombe, Geita na Simiyu,” alieleza Lukuvi.

Kuhusu ukusanyaji wa maduhuli, alisema hadi kufika Mei 15 mwaka huu, NHC ilikusanya Sh bilioni 79.7 sawa na asilimia 82 ya lengo la kukusanya Sh bilioni 96.6.

Alisema katika mwaka wa fedha 2021/22, shirika hilo limepanga kukusanya kodi ya pango kiasi cha Sh bilioni 105.6.

Join our Newsletter