Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 30Article 540643

Habari za Afya of Sunday, 30 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Naibu Waziri akiri mazingira yasiyo rafiki hedhi salama

WANAWAKE katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania wamekuwa wakikabiliwa na changamoto na mazingira yasiyo rafiki wakati wa hedhi hususani upatikanaji wa maji safi na salama.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama duniani ambayo huadhimishwa kila Mei 28.

Maadhimisho yamebeba kauli mbiu isemayo ni wakati wa kuchukua hatua ili kuhakikisha vifaa vya kujisitiri/taulo za hedhi zinapatikana kwa urahisi na bei nafuu kwa msichana au mwanamke.

“Kwa mujibu wa Shirika la Watoto Duniani (Unicef) na Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2013 linabainisha kuwa katika kila msichana mmoja kusini mwa jangwa la Sahara anakosa kwenda shule sababu ya kuwa kwenye hedhi,” alisema.

Alisema ,asilimia 52 ya vyoo vya wasichana havina milango na asilimia moja ya shule zimejenga shule kwa ajili ya wasichana kujisitiri wakiwa kwenye hedhi.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto, Ahmad Makuwani alisema lengo la kukutana katika maadhimisho hayo ni kujadiliana na kuvunja ukimya kwa kupaza sauti kwa jamii juu ya umuhimu wa hedhi salama.

Akitoa salamu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Fatuma Nasoro alisema ni wakati wa kuchukua hatua kuhakikisha kunakuwapo hedhi salama kwa wanawake na watoto wa kike.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Hedhi Salama kutoka wizarani, Salavata Silayo alisema lengo la jukwaa hilo ni kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana wakati wa hedhi na kuwawezesha kuwa na uelewa juu ya hedhi salama.

Mmoja wa washiriki wa maadhimisho hayo, Babu Ally alisema wanaume ni ngumu kuzungumzia hedhi kutokana na utamaduni uliojengeka kuwa suala hilo linamhusu mama pekee na si baba.