Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540253

xxxxxxxxxxx of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Nchimbi: Naanza kuhubiri Injili

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Rehema Nchimbi amesema kwa kuwa amestaafu utumishi wa umma kuanzia sasa ataelekeza nguvu katika kumtumikia Mungu na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alitangaza hayo wakati akimkabidhi ofisi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Binilith Mahenge aliyehamishiwa mkoani hapo hivi karibuni. Awali, Dk Mahenge alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

Nchimbi anakuwa mkuu wa mkoa mstaafu wa pili kwa hivi karibuni kutangaza kumtumikia Mungu kwa kuhubiri Injili.

Mwingine ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri ambaye amekuwa mwinjilisti wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) baada ya kustaafu mwaka jana.

Dk Nchimbi alisema sasa yupo huru kumtumikia Mungu kwa kuhubiri Injili na kuipigania CCM akiwa kada wa chama hicho.

“Asanteni sana wana-Singida kwa ushirikiano maana kwa kipindi chote nilichokaa hapa, sikuwa peke yangu. Kupitia kwenu viongozi niwashukuru pia wananchi wote wa mkoa huu,” alisema.

Akaongeza: “Hakika tuliishi vizuri ndio maana leo najivunia kustaafu kwa heshima kwani kwenye safari ndefu kama hii kuna kutumbuliwa pia.”

Dk Nchimbi alimshukuru Mungu, Rais Samia Suluhu Hassan na marais waliomtangulia kwa kumwamini na kumpa fursa ya kutumikia Watanzania akiwa kiongozi.

Alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida tangu mwaka 2016 na pia, amewahi kuongoza mikoa ya Dodoma na Njombe.

Alimuomba Dk Mahenge aendelee kuiboresha Singida kwa kutumia mikakati ya kiuchumi ili iwe na maendeleo yanayofanana na ya Mkoa wa Dodoma yalipo makao makuu ya nchi.

Kwa upande wake, Dk Mahenge alisema yeye ni muumini wa uchumi, hivyo atahakikisha anaiinua Singida kiuchumi.

“Lakini hakuna uchumi bila kilimo. Ni jukumu la kila kiongozi na kila mtendaji kuhakikisha kilimo kinatiliwa maanani,” alisema.

Akaongeza:“Nipeni ushirikiano wenu, vitendea kazi vyangu vyote ikiwa ni pamoja na rasilimali watu nimeviacha Dodoma, hivyo ninyi viongozi na watendaji tushikamane ili tuweze kumtumikia mwananchi wa Singida na kutimiza ndoto na matamanio ya Rais wetu.”

Awali akizungumza na HabariLEO, Dk Nchimbi alisema alipofika Singida sifa aliyoikuta ni kuwa ulikuwa mkoa wenye njaa, masikini na wenye ukame.

“Nilichokifanya ni kukataa kwamba Singida si mkoa wa njaa, ukame wala umasikini. Nilisema Singida ni mkoa ulio jirani na Mkoa wa Dodoma ambao ni makao makuu ya nch,i hivyo lazima Singida uuhudumie Mkoa wa Dodoma.”

“Nilihakikisha vijana hawaukimbii Singida na nilichofanya ni kuanzisha kilimo cha zao la korosho, ”alisema Dk Nchimbi.

Alisema hadi anastaafu, aliacha mipango ya kujengwa viwanja vya michezo katika Halmashauri ya Singida.

Alisema hadi anastaafu, alifanikiwa pia kubadilisha mtazamo wa wananchi wa Mkoa wa Njombe kutoka kutegemea kilimo cha viazi mviringo kama zao pekee la biashara, na kuanzisha kilimo cha parachichi.

Alisema alianziasha amri 13 za parachichi na anawashukuru wananchi wa Njombe walimwelewa na sasa wanaona matunda yake.

“Kwa kuwa Njombe kuna baridi kali nilibadili sare za wanafunzi wakavaa suruali badala ya kaptura na sketi na pia, walianza kuvaa sweta na wakati mwingine kofia baridi inapokuwa kali,” alisema.

Alisema katika Mkoa wa Dodoma, alileta utulivu wakati wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) walipotaka kufanya vurugu.

Dk Nchimbi pia anajivunia kuanzisha kilimo cha umwagiliaji Bwigiri, Kondoa, Mpwapwa sanjari na kuanzisha kilimo cha korosho Mpwapwa na kilimo cha bustani Chikopelo katika Wilaya ya Bahi.

Join our Newsletter