Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 05Article 545476

Habari Kuu of Monday, 5 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ndalichako: Mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo lipeni

Ndalichako: Mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo lipeni Ndalichako: Mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo lipeni

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu warejeshe ili iwanufaishe wahitaji wengine.

Alisema hayo Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mwongozo wa uombaji mikopo kwa mwaka 2021/2022iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) kwa kufuta tozo ya asilimia sita ya kulinda thamani ya mikopo iliyokuwa inatozwa kwa wanufaikam” alisema.

Akaongeza: “Naomba niwasihi sana wanufaika wote wa mikopo hii kufanya marejesho ili fedha mtakazorejesha ziendelee kuwanufaisha vijana wengine wenye uhitaji," alisema.

Mei Mosi mwaka huu akiwa katika sherehe za Mei Mosi jijini Mwanza, Rais Samia alielekeza kufutwa tozo ya kulinda thamani ya mkopo hiyo ili kupunguza mzigo kwa wafanyakazi.

Aidha, Mei 4 mwaka huu wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia bungeni jijini Dodoma, Profesa Ndalichako alielekeza kufutwa kwa adhabu ya asilimia 10 kwa wanufaika ambao hawajaanza kurejesha mikopo iliyoiva.

Kuhusu utoaji mikopo hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Profesa Ndalichako alisema serikali imetenga Sh bilioni 570 zitakazowanufaisha zaidi ya wanafunzi 160,000.

Alisema kati ya wanafunzi hao, wa mwaka wa kwanza wanatarajiwa kuwa 62,000 na wanaoendelea na masomo ni 98,000.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdul-Razaq Badru alisema maagizo hayo yametekelezwa na kuanzia Julai Mosi, mwaka huu taarifa binafsi za madeni hazina tozo na adhabu.