Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 26Article 539926

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ndugai: Fedha halmashauri zenye hati chafu zitazamwe upya

Ndugai: Fedha halmashauri zenye hati chafu zitazamwe upya Ndugai: Fedha halmashauri zenye hati chafu zitazamwe upya

SPIKA Job Ndugai ameishauri serikali kuangalia upya utaratibu wa kutopeleka fedha za maendeleo kwa halmashauri zenye hati chafu na kusisitiza uamuzi huo ni kuwatesa Wananchi.

Ndugai aliyasema hayo kutokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christine Mnzava (CCM).

Alisema hatua ya kutopeleka fedha za maendeleo kwenye halmashauri kwa kigezo cha hati chafu ni kuwanyima haki wananchi kwa makosa ya watendaji.

“Waziri wa Fedha, (Dk Mwigulu Nchemba) kabla hujaingia bungeni, Mheshimiwa Mnzava ameuliza swali kuhusu Hospitali ya Msalala. Lakini ni vyema utaratibu wa kuzinyima fedha sijui halmashauri zenye hati zenye mashaka; sijui hati chafu uangaliwe upya.”

“Mfano Mkoa wa Dodoma halmashauri zote isipokuwa halmashauri ya jiji, Singida halmashauri zote isipokuwa manispaa, Mkoa wa Tabora halmashauri zake zote isipokuwa manispaa zote hizi hazipelekewi fedha,” alisema.

Akaongeza: “Huu utaratibu uangaliwe upya maana unawanyima haki wananchi wakati ambaye hakuwasilisha vocha ni mhasibu. Tupeleke fedha za maendeleo, lakini mkiwachukulia hatua watendaji.”

Spika Ndugai aliitaka serikali kuangalia upya utaratibu wa kuzirejesha fedha za miradi ya maendeleo pindi zinapokuwa hazijatumika ndani ya mwaka husika.

“Leo Mei mnapeleka halmashauri Sh bilioni moja kwa ajili ya kujenga shule, mnajua kuna taratibu za manunuzi mwezi ujao mnazichukua au yuko huko mbali akuandikie wakati unajua zile fedha za miradi ya maendeleo, serikali muangalie utaratibu huu,” alisema.

Awali, katika swali la msingi, Dk Mnzava alitaka kujua serikali itazirejesha lini fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Msalala zilizorudishwa na mfumo baada ya Mwaka wa Fedha 2019/2020 kuisha.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Festo Dugange, alisema katika mwaka wa fedha 2019/20 Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ilipatiwa Sh milioni 500 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri.

“Hadi Juni 30 mwaka 2020, halmashauri hiyo ilikuwa imetumia Sh milioni 22.4 pekee na hivyo Sh milioni 477.59 zilirejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake za Mwaka 2015,” alisema.

Alisema katika mwaka wa fedha 2020/21, serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Sh bilioni moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa hospitali.

“Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa awamu hadi ujenzi wa hospitali hiyo utakapokamilika,”alisema.

Aidha, Dk Dugange alitoa mwito kwa wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanafuata sheria hiyo kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pindi wanapopelekewa fedha na pia kuomba kibali maalumu cha kutumia fedha hizo kama muda unaisha.

Join our Newsletter