Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540250

Habari Kuu of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ndugai akataa majibu ya waziri

Ndugai akataa majibu ya waziri Ndugai akataa majibu ya waziri

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ameonesha kutoridhishwa na jibu la Wizara ya Madini lililoulizwa na Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (CCM) na kuitaka wizara hiyo kulijibu upya siku nyingine.

Ndugai alitoa uamuzi huo jana baada ya Naibu Waziri wa Madini, Profesa Shukrani Manya kutojibu swali hilo kwa ufasaha.

Katika swali lake, Mwambe alitaka kujua mipango ya serikali baada ya utafiti wa madini ya graphite katika kata ya Chiwata kukamilika.

“Ndio maana niliwaambia tusome majibu, sidhani kama Mheshimiwa Mwambe una sababu ya kuuliza maswali ya nyongeza kwa sababu hili swali halijajibiwa.”

“Kwa hiyo nalirudisha tena Wizara ya Madini mlijibu tutalipangia tarehe nyingine ambapo mtatakiwa mlijibu kwa ufasaha. Swali lilikuwa ni rahisi tu kwamba, mradi wa madini ya graphite utafiti umekamilika serikali ina mpango gani, sasa hapa mmepiga blabla kabisa,” alisema Ndugai.

Katika swali la msingi, Mwambe alitaka kujua mpango wa serikali baada ya kukamilika kwa mradi wa utafiti wa madini ya graphite kata ya Chiwata.

Awali akijibu swali hilo, Profesa Manya alisema mikoa ya Kusini mwa Tanzania ya Lindi na Mtwara imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya madini ya kinywe (graphite) ambayo ni ya kimkakati yanayohitajika kwa kiasi kikubwa kwa sasa duniani kutokana na matumizi yake kama malighafi za viwandani.

“Kutokana na uwapo wa hazina ya madini hayo, zipo kampuni nyingi zinazomiliki leseni za utafutaji na uchimbaji madini ya kinywe katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo mikoa ya Lindi na Mtwara.”

“Hadi sasa kwa nchi nzima kuna jumla ya leseni 68 za utafutaji, leseni 24 za uchimbaji wa kati na leseni moja ya uchimbaji mkubwa wa madini ya kinywe,” alisema.

Alisema katika kata ya Chiwata ambayo ipo Jimbo la Ndanda, wilayani Masasi kuna leseni mbili za uchimbaji wa kati zilizotolewa kwa kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited Oktoba 18, mwaka 2018 baada ya kukamilisha shughuli za utafiti.

“Kinachosubiriwa ni kampuni hiyo kuanza uchimbaji na uchakataji wa madini ya kinywe katika leseni hizo,” alisema.

Profesa Manya alisema mpango wa serikali ni kuona kampuni zinazomiliki leseni za utafutaji madini zinakamilisha shughuli za utafiti na kuomba leseni za uchimbaji mkubwa au wa kati.

“Uwapo wa leseni hizo utapelekea kuanzishwa kwa miradi ya uchimbaji ambayo italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika sekta ya madini,” alisema.

Aidha, Profesa Manya alisema uanzishwaji wa miradi hiyo utaiwezesha serikali kukusanya mapato zaidi, kutoa fursa za ajira kwa Watanzania hasa wanaoishi katika maeneo yanayozunguka miradi, uhaulishaji wa teknolojia, kuingiza fedha za kigeni na manufaa mengine kwa jamii.

Join our Newsletter