Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 17Article 551878

Habari Kuu of Tuesday, 17 August 2021

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Ni Dr. Massawe masaa 16 kila siku kazini

Dk Massawe alifanya kazi saa 16 kwa siku Dk Massawe alifanya kazi saa 16 kwa siku

Siku mbili kabla ya mazishi yake, imeelezwa kuwa Daktari maarufu ambaye alikuwa bingwa wa watoto wachanga katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Augustine Massawe (73) alifanya kazi saa 16 kwa siku.

Dk Massawe ameelezewa kuwa kwa kipindi cha nusu ya maisha yake aliyatumia kufundisha, kutoa huduma kwa watoto wachanga na watoto njiti.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Agosti 16, 2021 na Msemaji wa familia ambaye pia ni mtoto wa marehemu, Dk Furaha Agosti wakati wa misa maalum ya kumuaga daktari huyo iliyofanyika katika viwanja vya chuo kikuu cha afya shirikishi Muhimbili MUHAS.

“Baba aliipenda sana kazi yake alifanya saa 16 kwa siku akiondoka saa 12 alirudi saa 4 mpaka saa 7 usiku. Alihudumia watoto njiti, alienda kufundisha alirudi tena kuhudumu kutoa huduma kwa watoto ilikuwa furaha yake,” amesema Dk Furaha ambaye pia ni daktari wa magonjwa ya kina mama na uzazi.

Amesema marehemu atafanyiwa misa kesho kuanzia saa 4 asubuhi katika kanisa la St Gasper lililopo Mbezi Beach na baadaye mwili utasafirishwa kuelekea Kibosho, Moshi kwa ajili ya mazishi siku ya Jumatano.

Wakuu wa chuo cha MUHAS, wakufunzi na wanafunzi wameungana pamoja kumuaga Dk Massawe huku wakimuelezea kwa mifano namna alivyoitendea haki taaluma hiyo.

Daktari ambaye amefanya kazi na Dk Massawe tangu mwaka 2006, Hegla Naburi amesema uwezo alionao sasa ulitokana na mafundisho ya bingwa huyo.

Amesema tangu kifo chake Ijumaa, amekuwa akipigiwa simu kutoka kwa watu wa nchi mbalimbali aliofanya nao kazi.

“Alikuwa daktari mzuri sana, mwalimu, baba na mshauri aliyependa kuona watoto wachanga wanapata huduma nzuri mara zote. Alikuwa anapenda wanafunzi na alipenda mara zote kuona wanafunzi wanafaulu.

“Alipenda sana wagonjwa wake mara kwa mara aliwanunulia hata kina mama chakula kama walikuwa hawana ndugu na maziwa hayatoki, nimejifunza mengi sana kutoka kwake,” amesema Dk Naburi.