Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 26Article 544342

Habari za Mikoani of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Operesheni haramu yamponza meneja shamba la misitu

Operesheni haramu yamponza meneja shamba la misitu Operesheni haramu yamponza meneja shamba la misitu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro amemsimamisha kazi Meneja wa Shamba la Hifadhi ya Misitu Silayo Bukombe wilayani Chato, Thadeus Shirima, kwa kufanya operesheni ya kuwaondoa watu bila kuwa na kibali cha Katibu Mkuu wa wizara hiyo. Dk Ndumbaro ameunda timu ya kuchunguza operesheni hiyo na kuipa siku 14 kukamilisha kazi na kuja na taarifa rasimu.

“Kutokana na mamlaka niliyo nayo, namsimamisha kazi meneja wa shamba la misitu kule Geita, Thadeus Shirima kuanzia sasa ili kupisha uchunguzi na akaripoti makao makuu,” Dk Ndumbaro amewaambia waandishi wa habari jijini Dodoma.

Alisema Shirima amesimamishwa kupisha uchunguzi juu ya tuhuma zinazomkabili.

Alisema wizara yake imepata malalamiko kutoka kwa Mbunge wa Bukombe, Doto Biteko pamoja na wabunge wengine wakilalamikia operesheni hiyo ambayo haikufuata utaratibu.

“Meneja wa Shamba la Hifadhi ya Misitu Shirima amejichukulia madaraka mikononi bila kuwasiliana na bosi wake, lakini hakuwasiliana na katibu mkuu ambaye ndiye kamanda wa vikosi vyote vya uhifadhi, wanyamapori na maliasili,” alifafanua Waziri wa Maliasili na Utalii.

Alisema kitendo chake hicho hakiendani na falsafa ya Wizara ya Maliasili na Utalii wala falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Sisi kama wizara tunasisitiza sana uhifadhi lakini tunaheshimu sana maslani na haki za Watanzania kwa sababu ndio wenye nchi na wamiliki wa maliasili. Tumeshasema wananchi wakifanyiwa ndivyo sivyo na ukawepo ushahidi hatutasita kuchukua hatua kali,” alisema.

Aidha, Dk Ndumbaro amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo kupeleka meneja mwingine kushika nafasi hiyo na leo awe amefika kituo cha kazi.

“Haturuhusu wananchi kujichukulia sheria mkononi, lakini pia haturuhusu kiongozi kujichukulia hatua mkononi, watendaji wengine wajifunze kutokana na hilo,” alisema.

Alifafanua, “Sisi tunafanya operesheni, lakini baada ya kukaa na kushauriana na kuelewana. Hili halikufuata utaratibu. Oparesheni hazikatazwi lakini lazima zizingatie kanuni taratibu na miongozo na zinatakiwa kuwa na kibali cha Katibu Mkuu, operesheni hii haikuwa na kibali cha kamanda husika ambaye ni Katibu Mkuu.”

Dk Ndumbaro alisema kitendo cha kujichukulia madaraka mikononi ambacho amefanya meneja huyo kinaharibu sura ya wizara hiyo pamoja na falsafa ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, Dk Ndumbaro alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka timu ya watu katika eneo la tukio kufanya tathimini ambayo itaainisha mambo mbalimbali ikiwemo athari kwa wananchi na imepewa siku 14 kukamilisha kazi hiyo.

“Timu hii tumeipa muda wa wiki mbili ili ije na majibu ambayo yataonyesha kuwa nini chanzo cha tukio hili lakini pia athari zilizotokea zimeatahiri watu kwa kiasi gani na kuja na ushauri wa nini kifanyike,” alisema.

Naibu Waziri Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema watumishi wote wanatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria na si vinginevyo.

“Sisi kama wizara hatutakuwa na nafasi ya kuwalinda wale wote ambao wanafanya kazi bila kuzingatia kanuni za utumishi wa umma na kufanya mambo kwa matakwa yao binafsi. Katika hotuba ya bajeti waziri alieleza kuwa tayari watumishi 61 tumeshawafukuza kazi,” alisema Masanja.