Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 08Article 562087

Uhalifu & Adhabu of Friday, 8 October 2021

Chanzo: mwananchidigital

Polisi waliofukuzwa kazi walikuwa wakikimbiza magendo ya Sh30,000 - Sirro

Siomon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Siomon Sirro, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema tukio la polisi saba waliovuka mpaka na kuingia nchini Malawi lilikuwa la aibu na kufichua kuwa mali ya magendo waliyokuwa wakiyafukuza thamani yake ni Sh30,000.

Mbali na sakata hilo, Sirro amebainisha kuwa kuna changamoto kubwa ya upelelezi inayosababisha mlundikano wa mahabusu na kuwaagiza wanaosimamia madawati ya upelelezi kuhakikisha suala hilo linamalizika.

Sirro ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Oktoba 8, 2021 katika Shule ya Polisi Moshi (MPA) wakati wa mahafali ya kuhitimu mafunzo ya uongozi ngazi ya wakaguzi wasaidizi ambapo maofisa 2,030 walihitimu wengi wakiwa ni wasomi wa vyuo vikuu.

Miongoni mwa waliohitimu mafunzo hayo, mmoja ana shahada ya udaktari wa falsafa, 50 wana shahada ya Uzamivu, 19 wana stashahada ya uzamili na 1,792 wana shahada ya kwanza za chuo kikuu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Sirro amewataka wahitimu hao wawe wa kwanza kuonyesha uwezo wao, maadili na wasiwe wa kwanza kuonyesha udhaifu na kutoa mfano wa tukio la askari hao saba.

Septemba 15, 2021 polisi hao wakiwa na gari na silaha walivuka mpaka na kuingia Malawi ambapo walizingirwa na wananchi na kuokolewa na polisi wa nchi hiyo na tayari wamefukuzwa kazi.

“Juzi kuna senior nco (mwenye stesheni sajini) ametoka hapa amekwenda anaongoza askari wanne, watano ni msomi anakimbizana na mtu mwenye magendo na magendo yenyewe hata hayafikii 30, 000."

“Kaingia Malawi kaongoza askari saba anakimbiza magendo anajua amevuka mpaka anakwenda kwenye nchi ya watu wengine na gari ya polisi na silaha ya polisi. Inatupa tabu sana sisi viongozi. Huyu ni msomi ametoka senior NCO hapa anavuka mpaka kwenda nchi ya watu akiwa na silaha ni aibu sana. Ni aibu pia kwetu ambao tunasimamia jeshi,” amesema.

Katika kuweka msisitizo wa suala hilo ameswma, "sitegemei na sitarajii wewe ambaye ni msomi ni inspekta sasa ukaenda kufanya mambo ya hovyo hovyo. Unaweza leo ukafurahia kwamba umepata uinspekta kesho tukachukua uinspekta."

Sirro ameeleza kuwa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto ya kufanya upelelezi na kwamba hata Rais Samia Hassan Suluhu amewahi kulizungumza na kuwataka wahakikishe mashauri yanakwisha kwa wakati.

“Tuna challenge (changamoto) kubwa ya upelelezi. Rais amekuwa akisema. Wengine watakwenda kusimamamia madawati ya upelelezi. Wahakikishe mashauri yanakwisha kwa wakati."

“Tuhakikishe mlundikano wa mahabusu unapungua. Mhakikishe haki inatendeka. Hayo ndio maelekezo yangu," amsema Sirro katika hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo.

Kwa upande wake mkuu wa majeshi nchini (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amesema kwa sasa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (bila kutaja wapi), linakabiliana na vitisho vya uhuru na mustakabali na usalama wa Tanzania.

Kwa upande wake Hamza amesema hali ya uhalifu nchini imepungua lakini makosa ya kimtandao yanaongezeka kwa kasi nchini Tanzania.

“Sasa hivi makosa ya kimtandao na usalama wa kimtandao yameanza kuongezeka kwa kasi. Makosa haya ni hatari sana kwa ustawi wa nchi. Mengi yanadhalilisha utu wa mtu, yanachochea chuki miongoni mwa wananchi,”alisema.

Kamandanti wa Shule ya Polisi Moshi (MPA), Ramadhan Mungi amesema katika wahitimu hao 2,030 wapo wenye elimu ya chuo kikuu na wamepata mafunzo ya kukabliana na mapambano makali yenye kuhusisha milipuko na silaha za moto.