Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 30Article 554509

Uhalifu & Adhabu of Monday, 30 August 2021

Chanzo: MWANANCHI

Polisi wawashikilia watu 9 kwa madai ya ujangili Katavi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga

Jeshi la polisi mkoa wa Katavi kwakushirikiana na kikosi maalumu cha askari wa Hifadhi za Taifa (Tanapa) kutoka makao makao Arusha wamekamata watu tisa akiwemo raia wa Burundi wakiwa na meno matatu ya tembo, bunduki aina ya AK- UC-0045-1988 ikiwa na magazine moja na risasi 28 iliyokuwa ikitumika kufanyia vitendo vya ujangili.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga akizungumza na wanahabari leo Agosti 30, amesema watuhumiwa hao walikamatwa wiki moja iliyopita eneo la Magogo kata ya Stalike wakiwa wametengeneza kambi ya muda ndani ya hifadhi.

Amewataja watuhumiwa nane wanaodaiwa kukamatwa na silaha hiyo pamoja na jino moja la tembo lenye uzito wa kilo 20, kuwa ni Francis Geremano (40) mkazi wa Kigamboni, Leonard Mtende (43)mkazi wa Kawajense na Charles Ngonyani (48) mkazi wa Kichangani.

Wengine ni Gabriel Milambo (42) mkazi wa Kawajense,Philibart Libuma (30)raia wa Burundi na mkazi wa Mishamo,Agustine Silasi (190 mkazi wa Stalike, Peter Kasanda (30) mkazi Kawajense na Charles Matege (30) mkazi wa Shanwe.

“Walikuwa na pikipiki mbili, moja aina ya SUNLG iliyobeba nyama ya ngiri uzito wa kilo 35 na Fecon. Hamza Jonsia (28) mkazi wa Tulieni yeye amekamatwa Agosti 22, 2021 saa 3:00 usiku eneo la Mjimwema akiwa na vipande viwili vya meno ya tembo yenye uzito wa kilo 4.72 vikiwa kwenye mfuko wa Bob marley," amesema Kuzaga.

Kutokana na hali hiyo Kuzaga amewaonya watu wenye tabia hiyo kuacha mara moja. Naye Ofisa Mhifadhi kitengo cha sheria na ulinzi wa kimkakati wa Hifadhi ya katavi (Kanapa), Lameck Matungwa amesema silaha zinapoingia maeneo ya hifadhi huleta athari kubwa kwa wanyama wote na siyo tembo pekee kwakuwa wanategemewa kuwa vivutio vya hifadhi za taifa.

“Hivyo tunaomba ushirikiano wa wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba ujangili tunautokomeza na ifikie hatua tuseme ujangili Katavi sasa basi, nitoe rai hasa kwa wananchi wanaozunguka hifadhi watoe taarifa, mfano tuliowakamata wengi ni wa Mpanda,” amesema Matungwa.