Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 558949

Habari Kuu of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Pombe inavyozidi kuhatarisha usalama wa vijana nchini

Pombe inavyozidi kuhatarisha usalama wa vijana nchini Pombe inavyozidi kuhatarisha usalama wa vijana nchini

Licha ya Tanzania kuwa na Sheria ya vileo na sheria nyingine ambatani, matumizi holela ya pombe zenye asilimia kubwa ya kilevi yamekithiri mitaani na kusababisha madhara makubwa kwa jamii.

Mwaka 2017 Serikali ilipiga marufuku matumizi ya pombe za pakti maarufu kama viroba baada ya kubaini kukithiri kwa tabia za ulevi na uchafuzi wa mazingira, hata hivyo imebainika kuwa wafanyabiashara wa pombe sasa wamegeukia kwenye chupa ndogo za plastiki mithili ya chupa za vitakasa mikono (sanitizer) zinazouzwa kwa bei nafuu ya kati ya Sh500 hadi Sh2000.

Pombe hizo zina vilevi kati ya asilimia 35 hadi 43 na zinapatikana kirahisi kwenye maduka ya mitaani, vibanda vya wamachinga na hata kwenye vituo vya daladala na kugeuka mbadala wa bia zenye ujazo wa mililita 350 zenye kilevi cha asilimia 4.5 hadi asilimia 5 zinazouzwa kati ya Sh1,500 hadi Sh2,500.“Kwa kadiri unavyokunywa pombe yenye kilevi kikubwa ndivyo madhara yanavyozidi kuwa makubwa,” anasema Dk Mashombo Mkamba, mtaalamu wa afya anayefanya kazi katika mradi wa kupunguza madhara ya pombe na unyanyasaji wa wanawake.

Anaendelea akisema “kuna madhara ya haraka kama vile mtu kubadilika tabia, madereva kusababisha ajali barabarani, kutoa lugha za matusi, ugomvi na kujeruhiwa, pia yapo madhara ya muda mrefu ya kuathirika kwa ini, figo, ugonjwa wa kisukari, magonjwa ya akili na matatizo ya kijamii kama kutelekeza familia na ugomvi usiokwisha.”

Zina faida ya haraka

James Wiriki ambaye anamiliki duka la vileo jijini Dar es Salaam anasema pombe hizo huwapa faida ya haraka kwa kuwa wateja ni wengi kwa kuwa zinauzwa bei nafuu.

“Nikinunua katoni ya pombe aina ya (anaitaja kwa jina) yenye chupa 30, bei yake ni Sh54,000 lakini ninapokuwa na Sh27,000 naweza kupata nusu yake sawa na chupa 15 kili kukidhi mahitaji ya wateja wangu,” alisema Wiriki.

Naye Raphaeli Dominick anasema yeye na wenzake hununua vinywaji hivyo kidogo kidogo kutoka katika maduka ya vinywaji na kuweka katika vibanda vyao, akitolea mfano wa boksi la kinywaji (anajitaja) ambalo huuzwa kwa Sh48,000 likiwa na chupa 30.

Unapata kiasi unachotaja

Mkazi wa Mwananyamala na mtumiaji wa pombe hizo Ibrahim Hamis anasema, wamekuwa wakitumia pombe hizo kutokana na unafuu wa bei.

“Nikitoka hapa nilipo nikizunguka tu mtaa wa pili ninao uwezo wa kupima kiasi chochote nachotaka kulingana na uwezo wa wangu na aina ya pombe,” anasema Hamis.

Anasema yeye hutumia pombe yoyote kutokana na aina zilizopo muda huo, kwani ikitokea umekosa ya aina fulani basi unaweza kutumia nyingine.

Mkazi wa Kinondoni, John Tarimo anasema huwa anatumia pombe hizo hasa wakati wa mchana na jioni kutokana na hali ya uchumi badala ya kutumuia bia ambazo huuzwa kwa bei kubwa.

Alibainisha kuwa wakati mwingine huwa anakunywa ili mradi tu alewe, mfano akiwa na Sh2,000 anaweza kunywa pombe za kupima viglasi vinne au kichupa kimoja tofauti na kunywa bia moja.

Kwa ujumla watumiaji wengi wa pombe hizo wameishia kuharibikiwa kimaisha, akiwemo James Magabe (si jina lake halisi) ambaye sasa anashindwa kujitegemea na kurudi kwa mama yake mzazi Temeke jijini Dar es Salaam kutokana na ulevi uliokithiri.

Tabia hiyo imesababisha Magabe (52) atengane na familia yake yenye mke na watoto wao wawili wanaosoma sekondari.

Mkewe (jina linahifadhiwa) anasema tangu ameolewa na Magabe alikuwa na tabia ya ulevi, lakini iliendelea kukithiri kiasi cha kushindwa kufanya kazi na hatimaye kufukuzwa kwenye mashirika kadhaa aliyofanya.

Hutokana na viwanda bubu

Mkoani Kilimanjaro Wilaya ya Rombo katika vijiji vilivyopo maeneo ya mpaka mwa Kenya na Tanzania kumekithiri pombe zaidi ya aina 30 zinazotengenezwa kwenye viwanda bubu ambavyo vinasadikiwa kuwa ni vingi wilayani humo.

Pombe hizo zimekuwa zikihifadhiwa kwenye chupa zenye baadhi ya majina ya makampuni halali ili kuzihalalisha na huuzwa kati ya Sh500 au Sh600.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbomai, Andrew Sarita alisema hali ni mbaya kwenye maeneo mengi ya wilaya hiyo ambapo vijana na wazee wamekuwa wakijiingiza kwenye unywaji wa pombe hizo na kuzisahau familia zao huku majukumu mengi yakiwageukia wanawake.

“Hizi pombe zimekuwa na madhara makubwa sana kwenye jamii na nashagaa kwanini Serikali imeliachia hili jambo, maana viwanda bubu ni vingi na vimepelekea kupoteza mwelekeo wa vijana wetu,” alisema Sarita.

Mwenyekiti wa kijiji cha Urauri, Justine Shirima alisema yapo maeneo ambayo ni maarufu kwa viwanda bubu ambavyo vipo maeneo ya Kahe wilayani humo ambapo viwanda hivyo vimekuwa vikisambaza pombe hizo maeneo mbalimbali ambapo wanywaji wakubwa wa pombe hizo ni vijana na wazee.

“Yaani unakuta kwenye mitaa vijana wamekuwa kama wazee wakati mwingine kukiwa na shughuli mahali unawaza utapata wapi kijana ambaye atawakilisha wenzake, ipo haja ya Serikali kulivalia njuga jambo hili, hatuna vijana na hata vizazi vijavyo sijui vitakuwa vya namna gani,” alisema Shirima.

Mkoani Mbeya pia zipo aina tatu za pombe zinazosafirishwa kwa siri kutoka nchi jirani na kusambazwa mitaani.

Mmoja wa wauzajia ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema hawezi kufahamu pombe hizo kama zina madhara kwa kuwa hajawahi kupata malalamiko yoyote kwa wanaotumia pombe hizo.

“Kwa sasa nafikiri wengi wamemaliza kwenye maduka yao, kwa sababu ni mtu mmoja tu ndio anayezisambaza, pia kuzivusha mpakani, ila zikishaingia huku hakuna shida yoyote, na sidhani kama zina madhara,” alisema.

Naye mmoja wa vijana katika mtaa wa Soweto jijini Mbeya alisema inasemekana pombe hizo huongeza nguvu za kiume ndio maana wateja wengi ni vijana na wanaofanya kazi ngumu.

Mmoja wa wauzaji wa pombe amesema zipo aina tatu lakini pia zipo katika mgawanyiko kulingana na utofauti wa gharama zake.

“Hizo za kwenye katoni kama zikiwa 12 ni Sh24,000 zikiwa 20 ni Sh56,000 na za kwenye madumu wanapima glasi Sh1,000 hadi Sh1,500, sasa muuzaji ndiye atajua anafaidikaje lakini faida ipo,” amesema.

Amesema ili kuzipata inabidi hadi kumpata mtu anayesambaza kutoka mpakani mwa kuingiza Tanzania.