Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 14Article 585859

Habari Kuu of Friday, 14 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Prof. Mkenda ageukia mitaala elimu

Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema anatarajia kutafuta wataalamu wabobezi katika elimu wakiwamo wastaafu ili kupata mchango wao wa kuboresha elimu ikiwamo uboreshaji wa mitaala.

Prof. Mkenda amesema katika kufanya hivyo, atatenga wiki tatu kuzungumza na watumishi wa wizara na kupitia nyaraka muhimu ili kufanya uchambuzi ili kuboresha elimu na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.

Aliyabainisha hayo jana, jijini hapa wakati wa makabidhiano ya ofisi kutoka kwa mtangulizi wake, Prof. Joyce Ndalichako.

Mkenda alisema wizara hiyo ni nyeti, hivyo inatakiwa kutendewa haki kwa kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na watumishi.

“Wizara hii si ya kuchezea ni wizara nyeti sana. Ukiichezea inahitaji si kubadilisha badilisha mambo, tutalichanganya taifa,” alisema.

“Pia ili kufanya kazi vizuri, naomba ushirikiano na msiwe na nidhamu ya uoga pale mnapoona kuwa mambo siyo msisite kuniambia ukweli kwani nyie ni wazoefu wa wizara hii muhimu,” alisisitiza.

Aliwataka watumishi kutokuwa na nidhamu ya uoga badala yake wafanye kazi kwa bidii ili kuinua elimu nchini. Pia aliwataka kumkosoa pale wanapoona anakwenda kinyume.

Naye Prof. Joyce Ndalichako alisema wizara hiyo imeachwa kwenye mikono salama, hivyo watumishi wampe ushirikiano wa kutosha waziri mpya.

Ndalichako alimtaka Prof. Mkenda kusimamia vizuri miradi ya elimu ambayo serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuiendeleza ikiwamo ya ujenzi wa shule, vyuo na mabweni pamoja na shule za wasichana.

Ndalichako alisema hana hofu na Prof. Mkenda kwa sababu yuko vizuri katika suala zima la elimu.