Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 13Article 585397

Habari Kuu of Thursday, 13 January 2022

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Profesa Mkenda: Bashe ataimudu Wizara ya Kilimo

Profesa Mkenda: Bashe ataimudu Wizara ya Kilimo Profesa Mkenda: Bashe ataimudu Wizara ya Kilimo

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (pichani) amekabidhi ofisi kwa Waziri mpya wa Kilimo, Hussein Bashe huku alieleza kuwa amekabidhi kwa mtu anayejua vizuri wizara hiyo. Alisema hayo jijini Dodoma wakati akikabidhi ofisi kwa Bashe baada ya kuapishwa juzi.

Profesa Mkenda aliwashukuru watumishi wa wizara hiyo kwa ushirikiano waliompa na kuwaaga. “Nakabidhi ofisi kwa mtu anayejua wizara hii, maana nilipokuja hapa nilimkuta Mheshimiwa Bashe tumefanya kazi pamoja anaifahamu vizuri ofisi na mengi yaliyomo humu anayafahamu, nakutakia kila la heri kwenye utumishi wako,” alisema Profesa Mkenda ambaye amehamishiwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

“Mimi na Bashe tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa, kuna wakati mambo yalikuwa yakiwaka moto tunakutana haraka usiku ili kujadili na kutoka na msimamo mmoja,” alisema. Alisema kilimo ni changamoto kubwa lakini kwa sasa kipo mikono salama na kuwataka waliobaki kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuondoa baadhi ya changamoto zilizobaki. Aliwashukuru watumishi wa wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati wa utekelezaji majukumu yake.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi, Bashe alisema katika kipindi cha mwaka mmoja walichofanya kazi pamoja, misingi mizuri imejengwa ambayo yeye ataendelea kuifanyia kazi ili kuhakikisha kilimo kinasonga mbele.

“Tumefanya kazi mwaka mmoja ambao tumejenga misingi mizuri ambayo tutaendelea nayo sababu najua juhudi tulizofanya tufikie sehemu nzuri, tuna changamoto nyingi zinatukabili hivyo lazima tuzifanyie kazi, kwa kipindi cha mwaka mmoja nimepata ujuzi mkubwa kutoka kwako, hivyo nakuahidi hakuna kilimo bila teknolojia wala sayansi hivyo nitaendelea kukusumbua,” alisema Bashe.