Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 19Article 543385

Habari Kuu of Saturday, 19 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Profesa Ndalichako: Elimu ya Juu anzisheni mijadala kuboresha mitaala

Profesa Ndalichako: Elimu ya Juu anzisheni mijadala kuboresha mitaala Profesa Ndalichako: Elimu ya Juu anzisheni mijadala kuboresha mitaala

SERIKALI imeziagiza taasisi za elimu ya juu, kuanzisha mijadala kwa ajili ya kujadili namna ya kuboresha mitaala yao.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Joyce Ndalichako katika Kongamano la wadau wa elimu la kujadili mitaala kwa shule za awali mpaka sekondari.

Alisema “Naziagiza taasisi za elimu ya juu nchini, suala hili halihusu elimu ya msingi pekee. Linahusu pia elimu yetu ya kati na vyuo vya elimu ya juu, niwaelekeze taasisi za elimu ya juu muanzishe mijadala kama hii ya kupitia mitaala yenu, kupata maoni kwa wadau,”

Alisema mabadiliko hayo ya mitaala yanayotarajiwa kufanywa baada ya kupokea maoni ya wadau na kuyachakata yatakuwa ya sita, tangu nchi ilipopata uhuru mwaka 1964.

Alisema mabadiliko ya kwanza ya mitaala yalifanyika 1967, ambayo yalilenga kuondoa mitaala ya kibaguzi iliyowekwa na wakoloni, kisha kuweka mitaala ya kujenga uzalendo kwa kuzingatia falsafa ya ujamaa na kujitegemea ambapo mabadiliko ya pili yalifanyika 1979, yaliyolenga kuweka msisitizo kwenye elimu ya nadharia na vitendo.

“Mabadiliko haya ya mitalaa yalilenga kuweka msisitizo kwenye elimu ya nadharia na vitendo, hivyo masomo ya michepuo yalianzishwa rasmi. Ikiwemo mchepuo wa ufundi, kilimo na sayansi kimu. Nadharia hizi zilianzishwa kujenga stadi zitakazowezesha wahitimu nchini kujikwamua kiuchumi kutokana na falsafa hiyo,” alisisitiza

Ndalichako alisema, mabadiliko ya tatu yalifanyika 1997, yaliyozingatia matakwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1995 na Tume ya kufanya mapitio ya elimu iliyoongozwa na Hayati Jackson Makweta 1982.

“Mabadiliko ya nne yalifanyika 2005, ambayo yaliweka mkazo kwenye ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia ujenzi wa umahiri, ikiwemo kuanzisha somo la Teknolojia, Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

“Pamoja na uchopekaji wa masuala ya mtambuka kama vile elimu ya Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) na stadi za maisha na mazingira.

Aidha alisema mabadiliko ya mwisho yalifanyika 2014, ambayo yanatumika kuanzia 2015 hadi sasa.

“2014 mabadiliko makubwa yalifanyika katika mitaala, yalilenga zaidi katika ngazi ya mwanzo ya wanafunzi. Yalilenga katika kuboeresha ufundishaji mitaala ngazi ya awali na msingi. Msisitizo uliwekwa kujenga ujuzi na kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesbau maarufu KKK,” alisema