Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 10Article 584767

Habari za Mikoani of Monday, 10 January 2022

Chanzo: www.mwananchi.co.tz

RC Homera ataka madarasa 8 yakamilishwe kabla ya Januari 17

RC Homera ataka madarasa 8 yakamilishwe kabla ya Januari 17 RC Homera ataka madarasa 8 yakamilishwe kabla ya Januari 17

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amewataka mafundi kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa madarasa manane yanayojengwa kwa kiwango cha ghorofa yaliyobaki kwa upande wa Jiji la Mbeya ili wanafunzi wanapoanza shule Januari 17 mwaka huu wasipate changamoto yoyote.

Jumla ya madarasa 92 yanajengwa Jijini Mbeya kupitia mradi wa fedha za Uviko 19, ambapo hadi sasa madarasa 84 yamekamilika kwa asilimia 100, huku ujenzi ukiendelea kwa mengine nane yanayojengwa kwa kiwango cha ghorofa.

Akizungumza leo Januari 10 wakati wa ziara yake jijini hapa kukagua ujenzi wa madarasa hayo pamoja miradi mingine ya maendeleo, RC Homera amesema amefurahishwa na kazi nzuri waliyoifanya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya katika kusimamia ujenzi wa vyumba hivyo yenye ubora na kiwango.

Amesema kwa sasa kazi imebaki kwa mafundi wanaojenga madarasa hayo ya gholofa kuhakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuendana na muda waliopewa ili wanafunzi wanapofungua shule Januari 17 mwaka huu wakute kazi imeisha.

"Hizi ni akili kubwa kwa Rais wetu, Samia Suluhu Hassan ambaye ametoa fedha kwa ajili ya maendeleo, niwapongeze kwa kazi nzuri kamati ya ulinzi na usalama Wilaya, niwaombe sasa mafundi wanaojenga hayo madarasa manane ya kiwango cha gholofa kuhakikisha wanazingatia muda uliopangwa kukamilisha miradi hiyo," amesema RC Homera.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Iganzo, Cliff Gasper amesema shule hiyo ilikuwa na madarasa 29 kwa wanafunzi 1,116, ambapo vyumba sita vilivgoongezwa imefanya kuwa na ziada ya madarasa matatu.

"Changamoto tulizopitia ilikuwa ni ongezeko la bei ya vifaa vya ujenzi, lakini tunashukuru kupitia Sh120 milioni tumeweza kujenga vyumba sita na kufanya kufikisha madarasa 35 ambayo jumla ya wanafunzi 1265 wataweza kutumia na kubaki ziada vitatu" amesema Gasper.

Naye Diwani wa Kata ya Iganzo, Daniel William amesema fedha hizo zimesaidia kwa kiasi kikubwa kukamilisha ujenzi huo kwani michango pekee ya wananchi isingeweza kufanya kitu chochote na kwamba lazima wamshukuru na kumpongeza Rais.

"Ingekuwa ni michango tungetafutana wananchi, tusingeweza kufikia lengo, lazima tumuombee Rais wetu na kumuunga mkono kwa kazi yake hii ya kutuletea maendeleo wananchi wake," amesema William.