Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 18Article 558178

Habari za Mikoani of Saturday, 18 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

RC Makala atoa mwezi mmoja Machinga kupangwa

RC Makala atoa mwezi mmoja Machinga kupangwa RC Makala atoa mwezi mmoja Machinga kupangwa

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla ametoa muda wa mwezi mmoja kwa madawati ya uwezesha wananchi kiuchumi yaliyopo katika kila wilaya kuanza maandalizi ya kuwapanga upya na vizuri wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ kuanzia Jumatatu Septemba 20, hadi Oktoba 18, 2021

Makalla ametoa tamko hilo leo Septemba 17, 2021 wakati akizindua kitabu cha mpango wa kuwapanga vizuri wafanyabiashara hao jijini Dar es salaam.

Makalla amesema uwepo wa machinga katika maeneo hayo yasiyo rasmi yamekuwa na athari nyingi ikiwemo kusababisha msongamano wa watu, ajali, kuikosesha serikali mapato na hata kukwamisha juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Makalla amesema mpango huo umewashirikisha wadau wote ikiwamo wafanyabiashara hao jambo lililowawezesha kujua wapo wangapi katika kila wilaya.

Aidha, aliyataja makundi matano ambayo mpango huo utawagusa kuwa ni wafanyabiashara waliojenga vibanda juu ya mifereji na mitaro, wale walio mbele ya maduka ya watu na kusababisha wateja kushindwa kuingia na kutoka dukani.

“Wafanyabiashara waliopo katika hifadhi za hifadhi ya barabara yaani road reserve, wanaofanya biashara na kuzuia njia za waenda kwa miguu hali inayolazimu baadhi kugongwa na magari kwa kupita barabara kabisa na wale wanaofanya biashara mbele ya taasisi za umma, shule za msingi na sekondari,” amesema.

Aidha, ameiagiza ofisi ya mkuu wa mkoa kuendelea kuweka mabango ya katazo ya kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.

Amesema kila mkuu wa wilaya kuhakikisha madawati hayo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, yanaratibu wamachinga hao bila bughdha.

Aidha, Mwakilishi wa wamachinga, Steven Lusinde ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania, amesema utaratibu huo wa mkuu wa mkoa ni mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.

“Tumepokea agizo lako tutalifikisha kwa wenzetu kama lilivyo ili kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakuu wa wilaya.

“Tunaomba wakuu wa wilaya wazingatie hili kwamba kutupanga upya na kutupanga vizuri, kwa sababu kuna maeneo wanastahili kutupanga vizuri maana tupo maeneo sahihi na si upya,” amesema.

Amesema ni kweli wamachinga wamekiuka utaratibu kwa kufanya biashasha maeneo yasiyorasmi.

“Niwaombe wenzangu popote walipo nikiwa kama makamu mwenyekiti wa machinga Tanzania kwamba kwa maelekezo haya tuwe watulivu tuhakikishe tunajipanga vizuri,” amesema.