Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 23Article 573610

Habari Kuu of Tuesday, 23 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia: Tanzania ni sehemu salama, karibuni

Samia: Tanzania ni salama, karibuni Samia: Tanzania ni salama, karibuni

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imefanikiwa kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi vya corona, nchi ipo salama hivyo amekaribisha wageni wakiwemo watalii na wawekezaji.

Alisema hayo jana jioni jijini Arusha wakati anazindua hoteli ya Gran Melia Arusha yenye hadhi ya nyota tano.

Rais Samia alisema ugonjwa wa Covid-19 uliathiri sekta ya utalii na akatoa mfano kuwa mwaka 2020 idadi ya watalii waliotembelea Tanzania ilipungua kwa asilimia 59 kutoka milioni 1.5 mwaka 2019 hadi 620,867 mwaka huo.

Alisema idadi ya ajira katika sekta hiyo ilipungua na pia mapato kutoka sekta hiyo yalipungua kwa asilimia 72.5.

Rais Samia alisema jitihada za kuzuia na kudhibiti virusi vya corona kwa kuzingatia mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na utoaji wa chanjo zimewezesha kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi hivyo.

“Kwa kweli Tanzania ni miongoni mwa nchi chache zinazoendelea kupokea watalii katika hali ya usalama hata wakati janga la corona lenyewe. Kwa hiyo sasa tupo salama zaidi , aje mmoja, njooni wote Tanzania,”alisema.

Rais Samia aliwashukuru wamiliki wa hoteli hiyo kwa kuwekeza nchini na akasema huo ni uthibitisho wa uwepo wa mazingira mazuri ya sekta ya utalii hapa Tanzania.

Aliwaeleza kuwa kuna vivutio vingi Tanzania hivyo wanaweza kuja kuwekeza zaidi ili kuongeza idadi ya hoteli sita wanazomiliki sasa nchini.

Rais Samia alisema wamiliki wa hoteli hiyo wana hoteli kwenye zaidi ya nchi 40 duniani na wamewekeza nchini kwa zaidi ya miaka 15 na sasa wana hoteli Zanzibar, Serengeti mkoani Mara, Dar es Salaam na sasa Arusha.

Rais Samia alisema zaidi ya asilimia 32.5 ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa ikiwa na utajiri wa vivutio vya utalii ikiwemo misitu ya asili, fukwe za kisasa, kuna utalii wa utamaduni na utalii wa mali kale ukiwemo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Alisema taasisi mbalimbali za kimataifa zimekuwa zikitoa tuzo kwa vivutio vya utalii nchi ukiwemo Mlima Kilimanjaro, Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na vivutio vya Zanzibar.

Rais Samia alisema juhudi za kuutangaza utalii zimeiwezesha moja ya sekta zinazoongoza katika uchumi wa nchi na akabainisha kuwa mwaka 2019 Tanzania ilipokea watalii milioni 1.5 walioingiza Dola za Marekani bilioni 2.6

Alisema sekta hiyo ilitoa takribani ajira milioni 1.6 za moja kwa moja za zisizo za moja kwa moja hivyo Serikali ya Tanzania inathamini mchango wa sekta ya utalii kwenye ujenzi wa uchumi.

Rais Samia alisema serikali ina dhamira ya dhati kuendeleza sekta ya utalii na itaendelea kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya kijamii na kiuchumi ili kufanikisha hilo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damasi Ndumbaro alimpongeza Rais Samia kwa kazi anazofanya kuiboresha sekta ya utalii na akasema ilikuwa imelala lakini sasa inafanya vizuri.

Dk Ndumbaro alisema chanjo ya Covid-19 imeleta imani kwa watalii na sasa Tanzania inaonekana ni nchi salama na idadi ya watalii imeongezeka.

Alisema makala ya televisheni aliyorekodi Rais Samia imesikika dunia nzima na tayari wamepatikana wawekezaji wengi. “Lakini vilevile mheshiwa Rais umeboresha usafiri wa maji na wa anga”alisema Dk Ndumbaro.