Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 25Article 559690

Habari Kuu of Saturday, 25 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia aifumua Tanesco, Maharage Chande Mkurugenzi Mpya

Rais Samia aifumua Tanesco, Maharage Chande Mkurugenzi Mpya Rais Samia aifumua Tanesco, Maharage Chande Mkurugenzi Mpya

RAIS Samia Suluhu, ameendelea kuliboresha kwa kulifumua Shirika la Umeme nchini (Tanesco) baada ya kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ndani ya shirika hilo.

Hivi karibuni alimteua Januari Makamba, kuwa Waziri wa Nishati akichukua nafasi ya Dk Medard Kalemani

Katika uteuzi wa leo, Rais Samia amemteua Omari Issa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya Tanesco, kabla ya uteuzi huo alikuwa Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Utekelezaji wa Miradi (PDB).

Pia amemteua Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, kabla ya uteuzi huo Chande alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kanda ya Afrika Mashariki na Magharibi wa Multichoice Afrika. Chande anachukua nafasi ya Dk Tito Mwinuka

Aidha amemteua Felschemi Mramba kuwa Kamishna wa Nishati Jadidifu, kabla ya uteuzi huo Mramba alikuwa mshauri Mkuu wa kiufundi Tanesco.

Pia amemteua Hassan Seif Said kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Nishati Vijijini (REA) kabla ya uteuzi huo Said alikuwa Meneja Mwandamizi wa Kanda ya Mashariki Tanesco.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Jaffar Haniu inasema uteuzi huo umeanza rasmi Septemba 23, 2021.

Aidha amemteua Michael Minja kuwa Kamishna wa Petrol na Gesi, Wizara ya Nishati. Kabla ya uteuzi huo Minja alikuwa Mkurugenzi Mkuu Tipper.

Wakati huo huo Waziri wa Nishati Januari Makamba, ameteua wajumbe wa shirika la Tanesco ambao ni Nehemia Mchechu, Zawadi Nanyaro, Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmass Massawe, Balozi Mwanahidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim, Abubakar Bakhressa na Christopher Gachuma.

Kwa mujibu wa Makamba uteuzi wa wajumbe hao umeanza rasmi leo Septemba 25.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga amewahamisha watumishi waandamizi watano kutoka Tanesco kwenda Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambako watapangiwa kazi nyingine.

Waliohamishwa ni Mhandisi Khalid James – Naibu Mkurugenzi Mtendaji na Uwekezaji, Mhandisi Raymond Seya – Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usambazaji na Masoko, Mhandisi Isaac Chanje, Naibu Mkurugenzi Mtendaji Usafirishaji, Nyelu Mwamaja – Mkuu Kitengo cha Ununuzi na Amos Ndegi, Mwanasheria wa Tanesco.