Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 08Article 569209

Habari Kuu of Monday, 8 November 2021

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Rais Samia akutana na Mtendaji wa ALMA

Rais Samia akizungumza jambo na Katibu Mtendaji wa ALMA, Bi. Joy Phumaphi Rais Samia akizungumza jambo na Katibu Mtendaji wa ALMA, Bi. Joy Phumaphi

Rais Samia leo tarehe 8 Novemba, 2021 amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA), Bi. Joy Phumaphi, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia amemshukuru Katibu huyo na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali katika kukabiliana na malaria nchini pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Rais Samia amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali, ikiwa ni pamoja na uundwaji wa Mabaraza ya Malaria ngazi zote pamoja na kupitia Umoja wa Wabunge wa Tanzania walio katika mapambano dhidi ya Malaria (TAPAMA) ambao wanafanya kazi kubwa ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika majimbo yao.

Aidha, Rais Samia amemuomba Bi. Phumaphi kuisaidia Tanzania kupata teknolojia ya kisasa kuboresha vyandarua vinavyozalishwa nchini pamoja na kuwezesha viuadudu vya kibaiolojia kuweza kutambulika kimataifa ikiwa ni moja ya jitihada za kuwezesha Serikali kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa Malaria kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa ALMA Bi. Phumaphi amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano wake na ALMA na kumpongeza kwa jitihada mbalimbali anazochukua kukabiliana na ugonjwa wa Malaria nchini Tanzania.

Bi. Phumaphi amesema Tanzania ni moja ya nchi za kuigwa Afrika kutokana na mafanikio iliyoyapata katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, hivyo ALMA itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.