Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 14Article 542608

Habari Kuu of Monday, 14 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia ataka udhibiti tanzanite

Rais Samia ataka udhibiti tanzanite Rais Samia ataka udhibiti tanzanite

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Madini itengeneze mfumo wa kulinda madini ya tanzanite, itafute utambulisho mpya wa rasilimali hiyo na pia soko lake lisimamiwe na chombo kimoja.

Aidha, ameagiza kuondolewa kwa vikwazo na urasimu unaokwamisha kuanza kuchimbwa madini ya chuma Mchuchuma na Liganga.

Rais Samia alitoa maagizo hayo jana wakati akizindua kiwanda cha kusafisha dhahabu kilichopo Sabasaba, Ilemela jijini Mwanza.

“Ningependa wizara (Nishati) isimamie madini yetu yote, lakini moja ya eneo ningependa msimamie mgodi wetu wa tanzanite. Mungu aliipendelea Tanzania pekee yake dunia nzima. Ni madini yanayopatikana Tanzania tu, lakini kwa sasa ni kama yanachimbwa dunia nzima, ukienda majirani ipo na bara la Asia ipo nyingi tu, imesambaa duniani,” alisema na kuongeza:

“Tanzanite yetu itamalizika, inavyotumika sasa haipendezi kuna haja ya kukaa na kure-brand haya madini yetu na kuyapa jina la upekee.”

Rais Samia alisema pia kuna haja ya kuwa na mfumo wa kuidhibiti tanzanite ili inunuliwe na kumilikiwa chini ya mwamvuli mmoja na kuweka mfumo wa udhibiti wa namna ya kuyauza kwa uchache, kwa bei kubwa ikiwa na jina zuri ili Tanzania inufaike.

Pia aliagiza wizara hiyo ihakikishe madini ya chuma katika mgodi wa Mchuchuma na Liganga yanaanza kuchimbwa mara moja kwa kuondoa vikwazo na urasimu.

Alisema mwekezaji wa mgodi huo alipewa leseni ya uchimbaji tangu mwaka 2015 ikiwa ni takribani miaka 11 sasa, lakini hadi leo hajaanza kuchimba.

“Sababu ya ucheleweshaji huu, nusu ni sisi serikali kwa urasimu wetu, lakini nusu yeye mwenyewe mwekezaji. Tunavyofanya urasimu sisi anapumzika, anakaa tu (mwekezaji), ikumbukwe kuwa kwao ana makaa mengi ya mawe, isije ikawa ni mbinu tusichimbe wao kwao wauze. Naomba tuondoshe vikwazo vyote vya serikali tubakie tukimtazama yeye,” alisema Rais Samia.

Alisema sasa ni wakati wa kumalizana na mwekezaji huyo kwa kuhakikisha taratibu zote zinazingatiwa na endapo atashindwa kuanza mradi aondolewe atafutwe mwekezaji mwingine.

Rais Samia aliitaka Wizara ya Madini itenge maeneo ya wachimbaji wadogo ili wachimbe kwa wingi madini, pia kupunguza tatizo la ukosefu ajira.

Pia, aliagiza watu waliojichukulia maeneo ya uchimbaji bila kuyaendeleza wafuatiliwe na endapo itabainika hawana uwezo wa kuyaendeleza wanyang’anywe yagawiwe kwa wengine wenye uwezo wa kuyaendeleza.

Alikaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa kuwa Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali hizo yakiwamo ya shaba, almasi, dhahabu, makaa ya mawe, vito na

chuma.

Rais Samia pia aliiagiza Wizara ya Madini irekebishe tozo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa forodha inayotozwa kwa wafanyabiashara wanaouza dhahabu viwandani na wanaoingiza madini kutoka nje.

Kuhusu kiwanda cha kusafisha dhahabu, alisema umegharimu Sh bilioni 12.2 na ni mtambo wa kisasa wenye uwezo wa kusafisha kilo 480 za dhahabu zinazoweza kuongezeka na kufikia kilo 660 kwa siku kwa kusafishwa kwa kiwango cha asilimia 99.9.

“Wasiwasi wangu uko kwenye upatikanaji wa malighafi kama kwa siku ni kilo 480, ingawa ndani ya mtambo huu kuna mashine zinazosafisha kilo 80 kwa

siku, nina wasiwasi wa upatikanaji wa malighafi. Kama serikali tuna kazi ya kufanya kuwezesha wachimbaji wachimbe na malighafi ipatikane kwa wingi,” alisema Rais Samia.

Alisema kiwanda hicho kitaongeza mapato ya serikali kupitia mrabaha na ushuru wa huduma, kitatoa ajira 120 za moja kwa moja na ajira 400 zisizo za moja kwa moja, kitawezesha utunzaji wa tofali za dhahabu, pia utawezesha madini mengine kuanishwa na kuthaminiwa.

Alisema pia kiwanda hicho kitaisadia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanza kununua dhahabu kwa mujibu wa sheria na kuwezesha nchi kuwa na amana ya dhahabu.

Rais Samia pia alisema kiwanda hicho kitachochea shughuli za uchimbaji wa madini kwenye ukanda wa ziwa, kitachochea shughuli za kiuchumi kwenye jiji la Mwanza na kwamba wawekezaji wametenga Sh bilioni 346.5 kwa ajili ya kununua dhahabu.