Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 13Article 557224

Habari Kuu of Monday, 13 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais Samia katoa maagizo makali kwa Mawaziri nchini

Rais Samia Rais Samia

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka mawaziri aliowateua kufanya kazi kwa weledi na kwa haraka zaidi kwa sababu muda hautoshi na kusistiza kuwa anataka kuona matokeo.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliowateua Jumapili Septemba 12, Rais Samia amesema anataka kuona matokeo kutoka katika kila Waziri aliyemteua.

“Nataka mjipange upya kuona mnatoa huduma gani,” amesema Rais Samia. Kiongozi huyo wa Nchi alitumia fursa kuelezea kuwa katika kibindi cha mwiezi sita akiwa madarakani amekuwa akijaribu kuwa mkimya na mtulivu ili kusoma wizara zote zinavyo endeshwa na Mawaziri pamoja na Makatibu.

Hata hivyo Rais Samia alionyesha kusikitishwa na baadhi ya Mawaziri na Makatibu ambao walichukulia ukimwa na utulivu wangu kama udhaifu. “Kuna wengine walichukulia ukimya na utulivu wangu kama ni njia kama ni njia ya wao kufanya kazi…. Nataka niwaambie kipindi cha miezi sita nilikuwa najifunza na nimeona vipi nakwenda na nyie,” amesema.

Rais Samia amewakumbusha watendaji kuwa kuna aina mbili katika uongozi (uongozi unaotoa adhabu na uongozi unaotoa zawadi) na kutahadharisha kuwa serikali itaendeshwa kwa matendo makali sio maneno makali. “Namaanisha twende tukafanyekazi msinitegemee kukaa hapa kuanza kufoka ovyo ovyo nitafoka kwa kalamu,” amesisitiza Rais Samia.

Kwa upande mwingine Rais Samia amesema ataendelea kufanya mabadiliko katika wizara mbalimbali kulingana na utendaji.

Jumapili ya Septemba 12, Rais Samia alifanya uteuzi wa Mawaziri wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akiwafuta kazi mawaziri watatu. Alimteua Dk Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi akichukua nafasi ya Marehemu Elias Kwandikwa. Alimteua January Makamba kuwa Waziri wa Nishati akichukua nafasi ya Dk Medard Kalemani ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Rais Samia pia alimteua Dk Ashantu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari akichukua nafasi ya Dk Faustine Ndugulile ambaye uteuzi wake pia ulitenguliwa.

Kadhalika, Rais Samia alimfuta kazi Dk Leonard Chamuriho na kumteua Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi. Na amemteua na kumuapisha Dk Eliezer Feleshi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali akichukua mikoba ya Profesa Adelardus Kilangi ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.