Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 22Article 559123

Habari Kuu of Wednesday, 22 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

Rais Samia kuunda timu ya kuwainua wanawake nchini

Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika kumbi za Mkutano wa Wakuu wa nchi New York Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa katika kumbi za Mkutano wa Wakuu wa nchi New York

Rais Samia Suluhu Hassan ameunda timu ya wataalamu ambayo inaangalia namna bora kwa Tanzania kufanikiwa katika kupata usawa wa kijinsia wakati wa uongozi wake, na timu hiyo itatoa mapendekezo kadhaa ya kuwainua wanawake katika vita dhidi ya umasikini. Ameyasema haya katika Mkutano wa Wakuu wa nchi wa 76 unaofanyika mjini New York nchini Marekani, kuwa Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuna kuwepo na usawa wa kijinsia.

Ameeleza kuwa tangu amekuwa Rais ameendelea kuteua viongozi wanawake katika nafasi mbalimbali ambazo hazijawahi kushikwa na wanawake ili kuondokana na dhana ya kuwa kuna nafasi ambazo wanawake hawawezi.

“Hivi karibuni nimemteua Waziri wa Ulinzi ambaye amekuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi hiyo nchini mwetu, ili kuondokana na dhana kuwa wanawake wanaweza nafasi fulani tu,” amesema Rais Samia.

Maeneo ambayo timu hiyo inapitia ni pamoja na marekebisho ya Sheria kandamizi, Sera na Mikakati ya kuwasaidia wanawake katika kupata fursa kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ajira, elimu na nyinginezo za kuwainua kiuchumi kama vile kumiliki ardhi, kupata mikopo na nafasi za uongozi.