Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 19Article 572851

Habari Kuu of Friday, 19 November 2021

Chanzo: mwananchidigital

Rais Samia mgeni rasmi mkutano wa UWT Zanzibar

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais wa Tanzania, Samia Suhulu Hassan kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano uliondaliwa na Umoja wa Wanawake (UWT) Zanzibar kumpongeza kushika nafasi hiyo na kazi nzuri aliyoifanya kwa kipindi cha miezi sita.

Naibu katibu Mkuu wa UWT Zanzibar, Tunu Juma Kondo ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Novemba 19, 2021. Mkutano huo utafanyika kesho Novemba 20, 2021 viwanja vya Maisara mjini Unguja.

"Tangu kuanzishwa kwa UWT waasisi wake walikuwa wakipigania nafasi na haki mbalimbali za kumwezesha mwanamke kushika nafasi za juu katika masuala ya uongozi na utawala ndoto ambazo zimetimia hivi karibuni baada ya kupatikana Rais wa kwanza mwanamke,' amesema Tunu

Tunu amesema sio tu wanajivunia kuwa na Rais mwanamke bali wanaona fahari ya kuwa na kiongozi mchapakazi, mwadilifu, mbunifu na mzalendo.

“Zamani wanawake tulipata ugumu hata wa kupata nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi lakini hivi sasa tunamshukru Mungu tumepata,"

Amesema kwamba ndani ya kipindi kifupi akiwa madarakani ameonyesha uwezo na Kasi kubwa kiutendaji katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kuendeleza uhusiano wa Kimataifa yanayotoa fursa mbalimbali za kuinua uchumi wa Tanzania.

Amewaomba Wananchi na wanachama kujitokeza kwa wingi kumsikiliza na kupokea maelekezo ya Chama na Serikali ambapo ratiba ya mkutano huo inaonyesha kuanza saa 1:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana.

Naye Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni, Moudline Cyrus Castico, amesema Rais Samia ameonyesha uwezo wa asili wa mwanamke ambaye anapokuwa katika ngazi ya familia anakuwa kiungo muhimu hivyo wana matumaini makubwa naye.

Amesema, Rais Samia ameiheshimisha Tanzania kimataifa kutokana na juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.

“Miradi yote iliyoachwa na awamu ya Serikali iliyopita hivi sasa Rais Samia ameiendeleza kwa kasi kubwa hali inayoonyesha kwamba wanawake wakipewa nafasi wanaweza kuonyesha miujiza mikubwa ya kiutendaji.”, alisema Castico