Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 14Article 542485

Habari Kuu of Monday, 14 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais TEC atoa neno maziko ya Mzikandakaya

Rais TEC atoa neno maziko ya Mzikandakaya Rais TEC atoa neno maziko ya Mzikandakaya

RAIS wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga amesema marehemu Dk Chrisant Mzindakaya ni Tunu ya uzalendo uliotukuka inayotakiwa kuenziwa na Watanzania kwani bado inahitajika kwa ustawi wa taifa.

Alisema hayo jana wakati akitoa salamu za TEC kwenye ibada ya maziko ya mwanasiasa huyo mkongwe iliyofanyika katika Kanisa la Kristu Mfalme lililopo Jimbo Katoliki la Sumbawanga mkoani Rukwa iliyoongozwa na Askofu Mstaafu wa jimbo hilo, Damian Kyaruzi.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Spika wa Bunge, Job Ndugai, mawaziri wakuu wastaafu, John Malecela na Mizengo Pinda, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Godfrey Pinda, wabunge wa mikoa ya Rukwa na Katavi, wakuu wa mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.

Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mbeya, alisema namna nzuri kwa watanzania kumuenzi Mzindakaya ni kuendeleza na kudumisha yote mazuri aliyoyafanya.

“Namfahamu Mzindakaya kama mzalendo halisi alikuwa akiililia na kuitetea Nchi kwa moyo wa dhati... licha ya kushika nyadhifa mbalimbali hakuwa na majivuno wala dharau kwa mamlaka wala mtu yeyote kwa taifa ndio maana nasema ni urithi mkubwa kwa taifa hili na tunu ambayo inatakiwa kuenziwa,” alisema Askofu .

Akitoa salamu za Bunge, Spika Ndugai alisema taifa limempoteza mtu muhimu mpigania maendeleo ambaye kwa muda wote wa maisha yake aliutumia kulitumikia taifa hili kwa unyenyekevu na upendo wa hali ya juu.

Waziri Mkuu Mstaafu, Malecela alisema kwamba alimfahamu Mzindakaya kama mtu aliyesaidia maendeleo ya mkoa wa Rukwa na taifa kwa ujumla hasa wakati wa kutekeleza mradi wa kilimo cha mahindi wakati wa serikali ya Mwalimu Julius Nyerere ilipopendekeza mikoa ya kulima kilimo hicho.

Mbunge wa jimbo la Kwela, Deus Sangu ambaye ni Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa wa Rukwa na Katavi, alisema Rukwa imepoteza mwasisi wa siasa za mkoa huo ambaye alikuwa kiungo muhimu kwa wanasiasa vijana majukwani na wamepata mafanikio.

Mzindakaya alifariki Juni 7 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa akitibiwa maradhi ya moyo. Alizikwa nyumbani kwake eneo la Kilimani kata ya Majengo mjini Sumbawanga.