Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 28Article 544519

Habari Kuu of Monday, 28 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rais akemea vita ya biashara sekta binafsi

Rais akemea vita ya biashara sekta binafsi Rais akemea vita ya biashara sekta binafsi

SERIKALI imekemea vita ya kibiashara baina ya Watanzania na kueleza kusikitishwa na matumizi ya taasisi za umma kuharibu juhudi za kukuza soko la bidhaa la nje na ndani ya nchi.

Akifungua Mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) jana jijini Dar es Salaam, Samia alisema “Jingine nilitaka kuzungumza hasa na sekta binafsi ni vita vya kibiashara kati yenu, lakini vita ile wanaoutumiwa silaha ni taasisi zetu za serikali.”

“Inaweza kutumika TBS (Shirika la Viwango Tanzania) kushusha sifa za bidhaa za mwingine ili mwingine afanye biashara, mnatumia Tume ya Ushindani (FCC) kupigana. TBS kazi yenu ni kuangalia mtu kaleta kitu, kinafaa au kimefaa, kama hakifai hakifai si kutumiwa kuangusha wengine,” alisema Samia.

Alisema anafahamu kuna vita kubwa kati yao hasa kwenye eneo la uzalishaji wa vifaa sawa ambapo mtu mmoja anazunguka kwenda TBS kuongea vibaya kuhusu mwingine ili biashara yake ianguke huku ambaye bidhaa zake zinaangushwa ana bidhaa bora zaidi. “Mpunguze vita vya biashara kati yenu, tufanye haki.”

Rais Samia alisema kuna wakati alipita Qatar akaambiwa wanahitaji vitu vyote kutoka Tanzania lakini kuna taasisi ya nchini imesema bidhaa hizo hazifai kwenda huko ingawa wao wapo tayari. Aliwataka waache kumalizana na kuimaliza nchi.

Akizungumza baada ya kupewa nafasi ya kutoa neno katika mkutano huo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, alihimiza ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi kwani ndio njia pekee ya kuzikimbiza sekta hizo kwa pamoja katika kutatua changamoto na kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa sekta moja haiwezi peke yake.

Dk Mpango aliunga mkono eneo la utafiti hasa kwenye ujenzi wa viwanda na kushauri wataalamu waangalie namna ya kuhakikisha vitalu vya miti nchini vinakuwa kama njia ya kuimarika kiuchumi. Alitaka pia huduma za ugani upande wa kilimo cha miti, iangaliwe upya.

Alieleza kuguswa na ushauri wa kutazama upya mfumo mzima wa matumizi na mapato ya serikali na kusema anaamini hilo litasaidia kuainisha sekta mpya zilizojitokeza hivi karibuni na kuangalia vyanzo vingine vya mapato ikiwamo upande wa Diaspora na mapato ya kigeni.