Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 27Article 559771

Siasa of Monday, 27 September 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Rushwa ya ngono, pesa chanzo wanawake kutoshiriki siasa

Rushwa ya ngono, pesa chanzo wanawake kutoshiriki siasa Rushwa ya ngono, pesa chanzo wanawake kutoshiriki siasa

WANAWAKE kutoka sehemu mbalimbali Dar es Salaam wametaja vikwazo vinavyowanyima uongozi katika ngazi za chini ni uwepo wa vitendo vya rushwa ya ngono na ya pesa.

Baadhi ya wanawake hao ambao wengi waliwahi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya kata hadi wilaya, walikuwa wanatoa uzoefu wao namna wanavyopitia vikwazo katika mafunzo ya uongozi yaliyofanyika juzi Kipunguni.

Katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Sauti ya Jamii Kipunguni chini ya ufadhili wa Women Fund Tanzania Trust, wengi walisema waliingia kugombea nafasi za uongozi bila kujipanga matokeo yake mambo waliyokutana nayo ni kuombwa rushwa ya ngono na wengine pesa.

Miongoni mwa wanawake hao ni Asha Abdallah aliyesema aliwahi kugombea nafasi ya Umoja wa Wanawake CCM na udiwani na alichokutana nacho walimdharau kwa kumuona ana umbile dogo na aliambiwa ili apite anahitaji kulala na mmoja wa viongozi wa Kamati za maamuzi.

"Nilipojitokeza kugombea kuna baadhi ya watu waliniponda ila sikukata tamaa lakini kadiri fomu yangu ilivyokuwa inasogea ngazi za maamuzi kuna vikwazo hujitokeza, mimi nilikuwa sina fedha za kuwapa wale wanaume walitaka nilale na mmoja wa viongozi,"alisema.

Alisema aliambiwa kama hataki kulala na mmoja wa wale viongozi wa maamuzi basi na uongozi hakuna.

Kwa upande wake, Mariam Bhako aliyewahi kugombea nafasi ya udiwani na kukosa alisema kama mtu hana pesa ni ngumu sana kupata uongozi kwani alichokiona watu wanakuwa wameshapangwa.

Seya Kazadi alisema yeye aliwahi kubambikiwa kesi ya uuzaji wa dawa za kulevya na kwamba anafuga vibaka nyumbani kwake kisa kilichomtokea mara tu baada ya kuchukua fomu za kugombea nafasi tofauti kwa vipindi tofauti.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Seleman Bishagazi aliwahimiza wanawake hao kutokubali kujihusisha na vitendo vya rushwa na kwamba pindi wanapoombwa wapige simu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kupata msaada.