Uko hapa: NyumbaniHabari2021 11 22Article 573319

Habari za Mikoani of Monday, 22 November 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Ruwasa kutumia Tsh. bilioni 78 miradi ya maji

Ruwasa kutumia Tsh. bilioni 78  miradi ya maji Ruwasa kutumia Tsh. bilioni 78 miradi ya maji

Mkoa wa Pwani unatarajia kutekeza miradi minane ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 3.7 ikiwa ni mgao kutoka fedha za kukabili athari za Covid- 19.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Clement Kivegalo alisema hayo wilayani Mafia baada ya kutembelea miradi ya maji na visima.

Kivegalo alisema fedha hizo zitapitia Ruwasa ilipokea shilingi bilioni 78 za miradi ya maji. Kivelego alisema walipokea fedha hizo kutoka serikalini na watazisimamia na kutekeleza miradi husika kwa wakati.

"Agizo lililopo ni kila mradi usizidi shilingi milioni 500 na kwa mkoa wa Pwani umepata kiasi cha shilingi bilioni 3.7 kati ya shilingi bilioni 78 ambazo zimegawanywa pia kwenye mikoa mingine kwa ajili ya miradi iliyo chini ya RUWASA,"alisema.

Meneja RUWASA Mkoa wa Pwani, Beatrice Kasimbazi alisema asilimia 76 ya watu wanapata maji mkoani humo ikiwemo mjini wanapata maji kwa asilimia 84 na Vijijini asilimia 72.

Kasimbazi alisema bajeti ya mwaka huu wametengewa shilingi bilioni 21 ambapo bilioni 3.7 ni kutoka katika fedha za Covid-19, bilioni 15 kutoka mfuko wa maji na shilingi bilioni 2.9 ni kwa ajili ya miradi ya PBR.

"Tutahakikisha shule, zahanati, masoko, na sehemu za mikusanyiko inapata maji ili maeneo ya mikusanyiko,wananchi wananawa maji tiririka kama wataalamu wanavyoshauri na kupambana na ugonjwa wa Covid-19,."alisema.

Kasimbazi alisema agizo lililopo ni kuhakikisha ikifika Machi 2022 miradi hiyo iwe imekamilika na itoe huduma hivyo basi wamejipanga na mameneja wa wilaya na watendaji wake kutekeleza agizo hilo kwa vitendo.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Martin Ntemo aliishukuru RUWASA kwenda kutembelea miradi na visima vinne wanavyochimba mwaka huu ndani ya vijiji ambavyo wanategemea kuongezwa na kufikia visima 10.

Ntemo alisema kuwa viongozi wa vijiji na wananchi wanapaswa kulinda miundombinu na vyanzo vya maji ambapo huo ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kufikisha maji Vijijini na mjini.

Alisema watakaokwenda kinyume na hilo kwa kuchoma moto, kufuga mifugo ama kufanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji watachukuliwa hatua za kisheria.

Awali Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mafia, Clement Lyoto alisema mwaka huu wametenga milioni 50 kwa ajili ya kutafuta vyanzo vya maji vinne.