Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 27Article 540088

Habari Kuu of Thursday, 27 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI YAPATA BIL 323/- UMEME MTO MALAGARASI

SERIKALI YAPATA BIL 323/- UMEME MTO MALAGARASI SERIKALI YAPATA BIL 323/- UMEME MTO MALAGARASI

SERIKALI ya Tanzania imesaini mikataba miwili na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) yenye thamani ya Dola milioni 140 za Marekani ambazo ni sawa na Sh bilioni 323.4 za Tanzania kwa ajili ya mradi wa kufua umeme wa Malagarasi mkoani Kigoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba jana alisaini mkataba huo kwa upande wa Serikali ya Tanzania na AfDB iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika Mashariki wa benki hiyo, Nnenna Nwabufo.

Mkataba huo ulisainiwa jijini Dar es Salaam na mradi huo utatekelezwa kwa miaka mitano na utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 45.9.

Tutuba alisema gharama za jumla za mradi huo ni Dola milioni 144.1 za Marekani ambapo kati ya fedha hizo, Dola milioni 120 za Marekani zitatolewa kupitia dirisha la AfDB, Dola milioni 20 za Marekani zitatolewa kupitia Mfuko wa Pamoja wa Ukuaji Afrika ( Africa Growing Together Fund) na Dola milioni 4.1 zitatolewa na Serikali ya Tanzania.

“Utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Malagarasi ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya mwaka 2015 pamoja na vipaumbele vyake vya maendeleo vya serikali vilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 ya Tanzania ambayo inaongoza maendeleo ya uchumi wa nchi yetu,”alisema Tutuba.

Alisema mradi wa Magalarasi utahusisha

ujenzi wa kituo kipya cha uzalishaji wa umeme wa gridi wa megawati 49.5 chenye uwezo wa kuzalisha GWh 181 za umeme kwa mwaka, lakini pia utekelezaji wa mradi huo utaboresha usambazaji wa umeme katika mikoa ya magharibi mwa Tanzania ili kuchangia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii pamoja na kupunguza umasikini.

“Mradi huu utapunguza utegemezi wa uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta mazito na kupunguza upotevu wa umeme. Pia utahusisha ujenzi wa bwawa, barabara za kuingia eneo la mradi, madaraja, kambi za kudumu, ofisi na nyumba za wafanyakazi, zahanati, shule za msingi, mitambo ya elektroniki inayohusika na uzalishaji na usambazaji wa umeme na kupanda miti,”alisema Tutuba.

Kwa mujibu wa Tutuba, kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili kutaongeza kiwango cha fedha kilichotengwa na AfDB kwa ajili ya kufadhili miradi ya sekta ya nishati nchini kutoka Dola milioni 325.2 za Marekani hadi kufikia Dola milioni 465.2 za Marekani sawa na Sh trilioni 1.1 za Tanzania.

Alisema AfDB pia imeonesha nia ya kufadhili mradi mwingine wa kufua umeme wa Kakono mkoani Kagera utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 87.

Tutuba alisema pamoja na ujenzi wa kituo cha uzalishaji umeme, mradi huo pia utajumuisha ujenzi wa njia za usafirishaji umeme, upanuzi wa mtandao wa usambazaji umeme vijijini ambao utahusu upanuzi wa mtandao wa kusambaza umeme wa kilovoti 132

na ununuzi wa transfoma mpya 15.

Alisema mradi huo pia utaijengea Tanesco uwezo wa kitaasisi, usambazaji wa vifaa vya kuunganisha wateja 4,250 katika Wilaya za Kigoma, Kibondo, na Kasulu zikiwemo kaya 1,000 zenye kipato cha chini, zahanati nne na shule za msingi sita.

Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika Mashariki wa AfDB, Nwabufo alisema mradi wa uzalishaji umeme wa Malagarasi utasaidia upatikanaji umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kwa wananchi lakini pia kusainiwa kwa mkataba huo ni ushuhuda kwamba benki hiyo inashirikiana vizuri na Serikali ya Tanzania.

Nwabufo alisema asilimia 83 ya gharama za mradi huo inagharimiwa na AfDB.

Join our Newsletter