Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540706

xxxxxxxxxxx ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

SIKU YA BAISKELI DUNIANI  Baiskeli ina mchango mkubwa  kiafya na kimaendeleo

LEO ni Siku ya Baiskeli Duniani. Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliazimia kwamba Juni 3 ya kila mwaka iwe ni siku ya baisikeli duniani.

Azimio husika lilipitishwa mnamo mwezi Aprili mwaka 2018 na nchi wanachama 193 za umoja huo.

Baiskeli ni usafiri unaojali mazingira na matumizi yake yanaimarisha afya. Ni chombo cha usafiri ambacho ni rahisi kukitumia.

Ni chombo kinachouzwa kwa bei ambayo takriban kila mtu anaweza kumudu, ni kifaa cha uhakika na pamoja na yote hayo chombo cha usafiri unaozingatia ulinzi wa mazingira.

Baiskeli pia inatoa mchango katika juhudi za kuyafikia malengo ya milenia ya maendeleo endelevu. Matumizi ya baisikeli yanaimarisha elimu, yanajenga afya na pia ni kinga ya maradhi.

Pamoja na sifa hizo, chombo hicho cha usafiri kinahimiza hali ya kuvumiliana, uelewano, heshima na pia kinachangia katika kuleta utangamano wa kijamii na mahusiano ya amani.

Baiskeli ya kwanza duniani ilitengenezwa mwaka 1817 na raia wa Ujerumani, Karl Drais, askari wa msituni ambaye alikuwa na elimu ya Fizikia na Hesabu.

Mwaka huo, Drais aliiendesha kwa mara ya kwanza mashine hiyo aliyoipa jina ‘Laufsmaschine’, kwa mujibu wa wasifu ulioandikwa na Dk Gerd Hüttmann.

Mnamo Juni 12, 1817 Karl Drais aliiendesha baiskeli hiyo aliyoivumbua ya magurudumu mawili umbali wa maili tano kutoka katikati mwa Mannheim na kurejea katika muda wa chini ya saa moja.

Ilikuwa baiskeli isiyokuwa na vikanyagio (pedeli) lakini mtu alihitaji kutumia miguu yake kuisaidia kwenda mbele, ilikuwa yenye kasi kuliko kutembea.

Mnamo mwaka wa 1839, mhunzi mmoja wa nchini Scotland, Kirkpatrick Macmillan, aliunganisha makanyagio na gurudumu la nyuma. Kisha, vyombo hivyo vya usafiri vikabadilika sana.

Baadaye Mfaransa mmoja, Pierre Michaux pamoja na mwanawe Ernest, waliunganisha makanyagio na gurudumu la mbele na hivyo wakabuni chombo kilichoitwa velocipede kutokana na neno la Kilatini velox (yenye kasi) na pedis (mguu).

Chombo hicho kilikwenda kasi na ilikuwa rahisi zaidi kukiendesha.

Katika uvumbuzi wa kwanza, Drais alipovumbua baiskeli hiyo aliiita jina la Laufmaschine (mashine iliyokimbia Ujerumani) lakini vyombo vya habari viliiita ‘Draisine’ kutokana na jina lake.

Kilichomsukuma kuvumbua baiskeli hiyo kimeelezwa kuwa ilikuwa kukabiliana na mgogro wa kimazingira uliokuwa umetokea wakati huo.

Drais alitaka mbadala wa kutumia farasi ambao walikuwa wakitumiwa siku hizo.

Miaka miwili kabla ya uvumuzi wake, Mlima Tambora ulilipuka na kuibadilisha dunia kwa kuwa jivu la volkeno lilisababisha kutoonekana kwa jua mwaka 1816 na mwaka huo kupewa jina la “mwaka bila jua”, na kulitokea njaa kubwa duniani.

Farasi wengi walichinjwa kwa sababu palikosekana chakula cha kuwalisha na wakaliwa na wafugaji wao kwa kuwa nao pia walikuwa hawana chakula.

Katika nchi nyingi, baiskeli hutumiwa sana kwa usafiri kwa sababu hazisababishi uchafuzi wala kelele na zinawawezesha watu wanaosafiri mwendo mfupi kufika haraka kuliko wanaposafiri kwa gari.

Katika Afrika, Asia, na kwingineko, baiskeli zimetumiwa na watu kusafirisha vitu vingi sana sokoni.

Mara nyingi, baiskeli hutumiwa kubeba watu wawili au zaidi, huku watu wa ukoo na marafiki wakikalia chuma kinachounganisha sehemu za baiskeli au kukalia sehemu ngumu ya kuwekea mizigo.

Mahitaji ya wasafiri ambao hutembea kwa miguu au kuendesha baiskeli, ambayo ni idadi kubwa ya watu yanapuuzwa na mataifa mengi licha ya kwamba faida za kuwekeza katika usafiri wa kundi hili zinaweza kuokoa maisha, kusaidia kulinda mazingira na kupunguza umasikini.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya baiskeli duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa ajili ya siku ya baiskeli duniani kushughulikia mahitaji ya waendesha baiskeli na wanaotembea kwa miguu ni muhimu katika suluhu za usafiri na kusaidia miji kuimarisha hali ya hewa na usalama barabarani.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema mazingira salama ya kutembea na kuendesha baiskeli ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kiafya kwa watu masikini ambao hawana magari, kutembea na kuendesha baiskeli kunawapa mfumo wa usafiri ambao unapunguza hatari za kupata magonjwa ya moyo, baadhi ya saratani, kisukari na hata kufariki dunia na hivyo si tu kuna faida za kiafya lakini pia gharama zake ni nafuu na rafiki.

Mbali na gharama zake, matumizi ya baiskeli ni safi na yanajali mazingira na kwa hiyo ni usafiri endelevu. Aidha baiskeli inaweza kutumika kwa ajili ya kuimarisha elimu, afya na michezo.

Pia matumizi ya baiskeli yanachagiza ujumbe chanya kwa ajili ya matumizi endelevu na uzalishaji ambao hauna athari mbaya zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

Mwakilishi wa kikundi kinachoendeleza Jumuiya ya PorElClima, Victor Vinuales, alisisitiza kuwa baiskeli inaashiria teknolojia ambayo ni rafiki kwa hali ya hewa na kwa afya ya raia, na inasaidia kuongeza kile ilichofafanua kama furaha ya ndani ya miji.

Mtaalamu wa usafiri nchini Uingereza, Adrian Davis, anasema kwamba kuendesha baiskeli “humlinda mtu asipate ugonjwa wa moyo, kisababishi kikuu cha kifo na kifo cha mapema.”

Mtu anapoendesha baiskeli hutumia nguvu nyingi sana. Hutumia asilimia 60 hadi 85 ya nguvu zake zote, tofauti na zile asilimia 45 hadi 50 anazotumia anapotembea. Kwa kuwa miguu yake hailemewi na uzito mwingi, haielekei sana kwamba mifupa yake itajeruhiwa kama anapotembea au anapokimbia.

Isitoshe, uendeshaji wa baiskeli hufurahisha na hiyo ni faida nyingine ya afya. Uchunguzi unaonesha kwamba kuendesha baiskeli huchochea kemikali zinazoitwa endorphin kwenye ubongo.

Kemikali hizo zaweza kumfanya mtu ajihisi vizuri zaidi. Mbali na kumfanya mtu ajihisi vizuri, kuendesha baiskeli kunaweza kumfanya mtu awe na umbo zuri.

Jinsi gani? Gazeti la The Guardian la Uingereza linaripoti kwamba “mwendeshaji baiskeli atachoma kalori saba kila dakika, au kalori 200 kila nusu saa akisafiri kwa mwendo wa wastani.”

Juu ya manufaa ya baisikeli, kiongozi wa shirika la misaada la kimataifa la World Bicycle Relief, Dave Neiswander anaeleza kwamba, usafiri ni msingi muhimu katika kuleta maendeleo, na kwamba watu walio kwenye sehemu za mashambani mara nyingi wanatembea kwa miguu ili kufika wanakokusudia.

Hata hivyo, licha ya faida zote hizo watu mara nyingi hawaitilii maanani baiskeli kuwa kifaa cha kuleta maendeleo. Baada ya kupitisha siku ya baisikeli duniani, Umoja wa Mataifa unawataka wanachama waipe basikeli kipaumbele katika mikakati yao ya maendeleo sambamba na kuijumuisha katika maamuzi ya kisiasa na mipango ya kitaifa na kimataifa.

Mkurugenzi wa shirika la misaada la Bicycle Relief kanda ya Ulaya, Kristina Jasiunaite anasema baisikeli inatoa mchango mkubwa katika juhudi za kuleta maendeleo.

Bi Jasiunaite anasema baisikeli ni chombo cha kufanikisha malengo endelevu duniani. Lakini aghalabu huwekwa pembeni ya mipango ya miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi huyo anasema siku ya baiskeli duniani itasaidia kuhamasisha mwamko wa kutambua umuhimu wa baiskeli kijamii na kiuchumi.

Anaeleza kuwa siku hii pia itachangia katika kuonesha umuhimu wa usafiri wa baiskeli kwa kuhakikisha kwamba hakuna anayeachwa nyuma au anayeshindwa kwenda shule, hospitali au sokoni kwa sababu tu sehemu hizo ziko mbali kutoka kwake.

Shirika la misaada ya baiskeli la Bicycle Relief linautekeleza mpango wake wa shule kwa kugawa baiskeli kwa watoto wa shule hasa wale wanaoishi mbali na shule zao.

Kutokana na mradi huo mahudhurio shuleni yameongezeka kwa asilimia 28 kwenye sehemu za mashambani katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. Na ufanisi miongoni mwa watoto wa shule umeongezeka kwa asilimia 59.

Shirika hilo la misaada ya baiskeli pia linashirikiana na wakulima wadogo na wahudumu wa afya ili kuzitatua changamoto za usafiri kwenye sehemu za mashambani.

Mpaka sasa shirika hilo la misaada limeshagawa baiskeli 400,000 na pia limeshatoa mafunzo ya uhandisi wa baiskeli kwa vijana 1900 barani Afrika.

0685 666964 au [email protected]

Join our Newsletter