Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 04Article 540916

Habari za Mikoani ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

SMZ yatoa mwongozo uchimbaji mchanga

SMZ yatoa mwongozo uchimbaji mchanga SMZ yatoa mwongozo uchimbaji mchanga

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetoa mwongozo ambao utatumika kwa ajili ya kuchimba mchanga katika mashamba ya watu binafsi na ya serikali ili kuepuka athari za uharibifu wa mazingira.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Suleiman Masoud Makame wakati akitoa maelezo kuhusu hali ya upatikanaji wa mchanga na mazingira yake kwa ujumla.

Alisema Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa mchanga ambapo juhudi na mikakati inahitajika kwa ajili ya kuweka mwongozo mzuri wa upatikanaji wa mchanga.

Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni pamoja na mashimo yanayochimbwa mchanga kuhakikisha yanakwenda chini si zaidi ya futi tano ili kuepuka kuibuka kwa maji.

Alisema kumejitokeza uharibifu mkubwa katika baadhi ya mashimo yaliyochimbwa mchanga kutokana na kuibuka kwa maji, sababu ikiwa ni watu kuchimba mchanga kwenda chini zaidi ya mita tatu.

''Wizara ya Maji, Nishati na Madini tayari tumeweka mwongozo wa uchimbaji wa mchanga katika mashimo mbalimbali ikiwemo yanayomilikiwa na wananchi ambapo mtu haruhusiwi kuchimba mchanga kwenda chini zaidi ya mita tano ili kuepuka athari za mazingira,” alisema.

Alisema wizara imeruhusu shimo la Chechele na Donge kutumika kwa ajili ya kuchimba mchanga na kwamba utaratibu mzuri umewekwa kwa watu wa kawaida wanaohitaji mchanga pamoja na kampuni inazotekeleza miradi ya serikali na sekta binafsi.

Makame aliwaambia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba Zanzibar inakabiliwa na uhaba wa mchanga kutokana na kuongezeka kwa matumizi yake ikiwemo shughuli za ujenzi za wananchi wa kawaida huku asilimia kubwa ya mchanga ukitumiwa kwenye ujenzi wa miradi ya serikali, sekta binafsi na hoteli za kitalii.

Alisema rasilimali ya mchanga kwa kiasi kikubwa inapatikana katika Mkoa wa Kaskazini Unguja katika mashamba ya watu binafsi na ya serikali huku eneo la asilimia 80 la kisiwa cha Zanzibar likiwa na mazingira ya mawe na udongo.

Join our Newsletter