Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 28Article 540259

Habari Kuu of Friday, 28 May 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Sababu tembo kuvamia maeneo ya makazi zatajwa

Sababu tembo kuvamia maeneo ya makazi zatajwa Sababu tembo kuvamia maeneo ya makazi zatajwa

KUDHIBITIWA kwa vitendo vya ujangili kumesababisha kuongezeka kwa tembo katika mbuga za wanyama za Tsavo na Mkomazi hali inayosababisha wanyama hao kuingia na kuzagaa katika makazi ya watu katika wilaya za Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Cornel Apson akizungumza na HabariLEO jana alisema ili kuwazuia wanyama hao, serikali imepanga kuchimba mabwawa mawili makubwa ya maji katika wilaya hizo kama kivutio cha kuwabakisha wanyama hao katika mbuga badala ya kwenda kutafuta maji maeneo mengine.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Same, alisema serikali ya wilaya kwa kushirikiana na wabunge wa majimbo ya Mwanga na Same Mashariki waliomba msaada wa Wizara ya Maliasili na Utalii wa kukabiliana na changamoto hiyo, ambapo wizara iliwatuma Naibu Waziri wake, Mary Masanja na Katibu Mkuu, Allan Kijazi.

Alisema viongozi hao Jumamosi iliyopita walifanya ziara Same na Jumapili walikuwa Mwanga na miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni kujenga mabwawa katika wilaya zote ili kuwazuia tembo wasitoke mbugani.

Aidha, alisema serikali imeanzisha Jeshi Usu katika kata ya Toloha wilaya ya Mwanga ambalo litakuwa na jukumu la kudhibiti tembo wasitoke katika maeneo yao kwenda kwa wananchi kwa sababu athari yake ni kubwa.

Kwa upande wa Same, alisema serikali imepanga kupeleka kikosi kidogo katika kata ya Kisiwani ambacho pia kitakuwa na jukumu la kuwadhibiti wanyama hao wasiingie katika makazi ya watu.

“Kinachosubiriwa ni kuviongezea nguvu vikosi hivyo, ambapo baada ya Bunge la Bajeti waziri ataelekeza nguvu katika kuongeza askari, silaha na magari ili kurahisisha kazi hiyo,” alisema Apson.

Alisema katika mikakati iliyopitishwa wananchi watashirikishwa katika kuwafukuza kwa amani wanyama hao, ambapo watapewa vifaa vya kufukuza tembo kama vile vuvuzela kutokana na wanyama hao kutopenda kelele.

Alisema pia kutakuwa na utoaji wa elimu kwa wananchi ya namna ya kuishi na tembo bila kuleta madhara kwa sababu wanyama hao hawatakiwi kuuliwa.

Alisema kupitia mafunzo hayo wananchi watafundishwa tabia za tembo hali itakayowafanya waishi nao kirafiki.

“Mapendekezo mengine yaliyokubaliwa ni kuwa, wananchi wasiingize mifugo katika maeneo ya wanyama kwani wanyama kama tembo hawataki kusumbuliwa ndio maana wanaamua kutoka katika hifadhi kwenda mahali tulivu,” alisema.

Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Mwanga, zamani Wapare walikuwa wakiishi maeneo ya milimani katika wilaya za Mwanga na Same na eneo la tambarare lilikuwa ni hifadhi ya wanyama, lakini sasa wananchi wamejenga katika eneo la hifadhi na kuwalazimisha wanyama kuhama.

Join our Newsletter