Uko hapa: NyumbaniHabari2021 08 19Article 552409

Habari za Afya of Thursday, 19 August 2021

Chanzo: MWANANCHI

Sababu ya wanaume wengi kufanya tohara

Wanaume wengi kufanyiwa tohara Wanaume wengi kufanyiwa tohara

Imeelezwa kuwa baadhi ya wanawake wilayani Kahama mkoani Shinyanga kuwanyima unyumba waume zao kushinikiza wafanye tohara kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya VVU na saratani ya shingo ya mlango wa kizazi, kumeongeza idadi ya wanaume wanaotaka kutahiriwa.

Hayo yameelezwa na mratibu wa tohara manispaa ya Kahama, Hadji Sued leo Alhamisi Agosti 19, 2021 katika mkutano wake na wanahabari kwenye eneo la utoaji wa huduma ya tohara akibainisha kuwa baada ya mkakati huo wa wanawake, idadi ya wanaume wanaojitokeza kufanyiwa tohara inazidi kuongezeka kila siku.

Amesema wajawazito wamechukua hatua hiyo baada ya kupewa elimu ya kujikinga na maambukizi ya VVU na watoa huduma wafikapo kliniki kupata huduma ya afya ya uzazi.

Sued amesema kuanzia Januari hadi Julai 2021 wamewatahiri wanaume 335 na mwaka 2020 kuanzia Oktoba hadi Desemba walitoa huduma hiyo kwa zaidi ya wanaume 400.

Amesema mwaka 2020 waliweka malengo ya kutoa huduma ya tohara kwa watu 6,755 na walifika lengo na mwaka 2021 kuanzia Septemba wanatarajia kutoa huduma hiyo kwa vijana, watu wazima na wazee 14,000 ambapo kila mwezi watakuwa wanawafanyia tohara watu 1,170.

Sued amesema utoaji wa huduma hiyo imesaidia kupunguza wimbi la maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo ilikuwa asilimia 6.4.

Amesema mwaka 2010/11 Mkoa wa Shinyanga ulikuwa juu kwa maambukizi ya VVU kwa asilimia 7.4 na mwaka 2015/16 maambukizi yalipungua kwa asilimia 5.9.

Lukia Abdallah aliyefika katika hospitali ya manispaa amesema elimu ya tohara aliipata tangu akiwa anasoma elimu ya dini hivyo watoto wake wa kiume wote wamefanyiwa tohara.

Mwanamke mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina ameieleza Mwananchi Digital kuwa wakati anampeleka mwanaye kufanyiwa tohara aliambatana na mumewe ambaye alikuwa hajafanyiwa tohara na siku ambayo alimfanyia tohara mwanaye na mumewe naye alifanyiwa.