Uko hapa: NyumbaniHabari2021 09 24Article 559435

Uhalifu & Adhabu of Friday, 24 September 2021

Chanzo: TanzaniaWeb

"Sabaya hakupewa kibali kufanya kazi nje ya eneo lake la kazi" - Katibu Tawala

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya HAI, Ole Sabaya Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya HAI, Ole Sabaya

KATIBU Tawala Msaidizi wa zamani wa Mkoa wa Kilimanjaro, Renatus Msangira (45), amepanda kizimbani, akidai aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani humo, Lengai Ole Sabaya, hakupewa kibali chochote cha maandishi kwenda kutekeleza majukumu nje ya kituo chake cha kazi.

Msangira, ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, alitoa madai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha wakati akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Filex Kwetukia.

Sabaya na wenzake sita, wanakabiliwa na mashtaka matano, ya matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Washtakiwa wenzake katika shauri hilo la uhujumu ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha (29) na Nathan Msuya (31).

Mbele ya Hakimu wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda, alidai Sabaya hakuwahi kupewa kibali cha maandishi kwenda kutekeleza majukumu nje ya kituo chake cha kazi cha Wilaya ya Hai.

Alidai kiutaratibu Mkuu wa Wilaya akitaka kwenda kufanya kazi nje ya kituo chake cha kazi inatakiwa apate kibali cha maandishi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa, lakini hilo halikufanyika.

“Kwa kuwa mimi nilikuwa RAS Msaidizi ninayesimamia utawala na rasilimali watu katika Mkoa wa Kilimanjaro, kama Sabaya angekuwa amepewa kibali cha maandishi na RC kwenda kufanya kazi nje ya wilaya yake ningefahamu kwa kuwa kingepitia kwenye ofisi yangu kwa kuwa mimi ni msimamizi wa shughuli za kiutawala,” alidai shahidi huyo.

Msangira, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia utawala na mipango katika Wizara ya Fedha na Mipango, alidai kwamba awali alikuwa mtumishi katika Mkoa wa Kilimanjaro, kuanzia Machi 20, mwaka 2020 hadi Juni mwaka huo ndipo akahamishwa kupelekwa wizarani.

“Katika mazingira ya kawaida DC akitaka kutoka nje ya kituo chake cha kazi kwenda sehemu ya wilaya nyingine au mkoa mwingine kwenda kutekeleza majukumu ya kikazi, lazima aombe ruhusa kwa kiongozi wake wa Mkoa na apewa kibali cha maandishi,”’alidai.

Alidai katika kipindi cha Machi hadi Juni mwaka huu, Sabaya alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, lakini Mei 13, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alimsimamisha kazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Katika hatua nyingine shahidi huyo, alidai kwamba Mkuu wa Wilaya hapaswi kuwa na walinzi binafsi kwa kuwa anakuwa na ulinzi wa askari polisi akiwa kazini, nyumbani kwake na kwenye ziara za kikazi kulingana jeografia ya eneo husika.

“Kwa utaratibu wakuu wa wilaya,wakuu wa mikoa,mawaziri na manaibu waziri hawatakiwi kuwa na walinzi binafsi lakini kama kuna jambo la kuhatarisha usalama wake anaomba kibali kutoka katika mamlaka husika za usalama.

Aliieleza mahakama kwamba endapo Mkuu wa Wilaya atahitaji kuwa na walinzi binafsi tenda itatangazwa na mshindi ndiye atapatiwa shughuli ya kutoa huduma hiyo.

“Ulinzi wa kwenye makazi wanalinda askari polisi na kama DC anahitaji walinzi binafsi Katibu Tawala wa Wilaya (DAS), anaandika barua kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD),kuomba kuongewa walinzi binafsi kama wanahitajika.