Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 03Article 540760

Habari Kuu of Thursday, 3 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia: Nataka matokeo

Samia: Nataka matokeo Samia: Nataka matokeo

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo takribani saba kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa na kusisitiza anataka kuona matokeo mazuri ya utendaji wao.

Rais Samia alitoa maagizo hayo jana katika viwanja vya Ikulu, Chamwino, Dodoma wakati akiwaapisha makatibu tawala wa mikoa 11 na viongozi wa taasisi mbalimbali.

Maagizo hayo ni pamoja na kuwataka kusimamia maendeleo ya mikoa yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, kushirikiana wenyewe kwa wenyewe, kutatua migogoro, kuzingatia weledi, upendo na maadili na kusimamia mapato ya mikoa hiyo, pamoja na kusimamia miradi kwa manufaa ya wananchi.

“Ningependa mtambue kwamba majukumu yaliyo mbele yenu ni makubwa mno na wote tunawatazama nyie. Makatibu tawala wa mikoa mnakwenda kuwa washauri wa mikoa, viongozi wa sekretarieti ya mikoa na ni makatibu wa kamati za usalama za mikoa,” alisema Rais Samia

Alisema makatibu hao tawala ni watendaji wakuu wa serikali katika mikoa, wasimamizi wa shughuli zote za kiutendaji katika mikoa, maofisa masuhuli wa mikoa na watumishi wa umma kwenye mikoa hiyo.

“Maana yake ni kwamba watumishi wote wa serikali katika mikoa wako chini yenu na shughuli ya kuongoza au kuchunguza watumishi wa serikali ni kubwa,” alisema Rais Samia.

Alisema pia, makatibu tawala ni kiungo muhimu kati ya serikali za mitaa na serikali kuu. “Watendaji wote wa wilaya wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri (DED) wako chini ya makatibu hao tawala hivyo matumizi mazuri au mabaya yakitokea wao ndio wanahusika,” alisema.

Kuhusu uteuzi wa asilimia 46 ya wanawake katika nafasi za makatibu tawala, Rais Samia alisema alichukua uamuzi huo si kwa sababu ni wanawake, bali kwa sababu wana uwezo wa kufanyakazi.

Alieleza uteuzi wa MaRas na Ma-RC katika mikoa yote nchini unaonesha ni namna gani hali itakavyokuwa katika maeneo yao, huku akitolea mfano Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Albert Chalamila na RAS wake, Ngusa Samike kuwa mjumuiko wao ni kama kibiriti na petroli.

“Ngusa mkimya lakini mwenzake ni mlipukaji, sijui kutakuaje lakini nataka mjue kuwa si hawa tu ila wote tunawaangalia,” alisema.

Aliagiza kuwa mikoa ambayo wamepangwa RC na RAS wote wanawake hataki kusikia migogoro na endapo itatokea hivyo watakuwa wamemtia aibu yeye (Rais) pamoja na wanawake wote kwa ujumla.

“Ile mimi usinibababishe sitaki kusikia. Pale nyie si wanawake ni Mkuu wa Mkoa na RAS wako na hakuna sababu ya kwenda kupapurana, mkienda kufanya hivyo mnanitia aibu mimi maana yatakayoenda kusemwa ndio shughuli ya wanawake. Tulijua tu wanawake wawili hawakai pamoja, kwanini msikae pamoja mbona mnaolewa wawili mnakaa pamoja kwa

nini kwenye kazi msikae pamoja,” alisema Rais Samia.

Alisema mikoa yenye mkuu wa mkoa na katibu tawala mwanamke ndio anayoitegemea na kwa wakuu wa mikoa waliowekewa Ma- Ras wanawake watambue kuwa, wanawake ni wafanyakazi na wasomi hivyo wafanye kazi kwa ushirikiano.

“Sasa mkienda huko sitaki kusikia eti usinibabaishe wewe si mwanamke tu! aliyekuambia nani mwanamke ni tu, wewe ulizaliwa na nani, ulikutwa na nani na sasa unakuzwa na nani, aliyekufanya uitwe baba ni nani?” alihoji Rais Samia.

Alisema hataki kusikia mambo ya kudharauliana zaidi ya kusikia viongozi hao wanafanyakazi bila kubaguana kwa kigezo chochote iwe, jinsia, imani au itikadi kwani kila mtanzania ana haki ya kuchangia katika maendeleo ya Tanzania.

Alisema hataki kusikia yaliyompata aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjro, Anna Mghwira yampate Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga kwa

kuwa ametoka chama cha upinzani.

“Walikuwa wakidai etu si mwenzao, katokea wapi na kwamba aliyempeleka kule alikosea. Nasema hivi Rais hakosei,” alisema Rais Samia.

Aliwataka viongozi hao watatue kero za wananchi, wasimamie haki na migogoro ikiwamo ya ardhi na mirathi ambayo iko mingi na kuwaumiza zaidi wanawake.

Rais Samia pia aliwataka wazingatie maadili kwa kutojiingiza kwenye migogoro hasa ya ardhi au kujimilikisha ardhi kinyume cha sheria.

“Kulikuwa na mgogoro mmoja Tanganyika, mkuu wa wilaya kaenda kujimilikisha eka kadhaa kalmia, Mungu kamuitikia anatakiwa kulipa pale anapopitisha mazao halipi, sasa DC huyu unamuacha wa nini? mkuu wa mkoa au RAS atakayejiingiza kwenye hayo vyombo vipo vitaona,” alionya.

Aliwataka kupitia nafasi yao ya uafisa masuhuli kusimamia matumizi mazuri ya serikali. “Kama kuna miradi

iendane na thamani ya fedha inayotumika. Tumechoka kufika pale kufungua mradi unafika Rais ndio inabidi asimame akahesabu matofali na mabati aone kwamba thamani inaendana na pesa iliyotajwa. Hili sasa hapana,” alisema Rais Samia.

Rais Samia pia aliwataka viongozi hao kusimamia, kurekebisha na kutatua mambo yote ya ajabu kwenye mikoa yanayohusu utumishi wa umma ikiwamo uhamisho wa hovyo, watu kutopandishwa vyeo na upendeleo uliokithiri na kutaka kila mtumishi apate haki yake kama sheria za ajira zinavyosema.

Alikemea kitendo cha uzembe uliokithiri kwa watumishi wa umma ikiwamo utoro wa kutokwenda kazini na pindi wanapochukuliwa hatua kukimbilia kukata rufaa Tume ya Utumishi wa Umma.

“Kuna mambo kama haya yanaendelea huko mikoani wakuu wa mikoa wapo, Ma-RAS wapo na wengine wapo. Sasa itakapopokea tena mafaili ya aina hiyo, watu wanakata rufaa za kipumbavu mimi na nyinyi,” alisema Rais Samia.

Walioapishwa jana ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu

George Mkuchika, Makatibu Tawala wa Mikoa, Balozi Batilda Burian (Shinyanga), Doroth Mwaluko (Singida), Samike (Mwanza), Rodrick Mpogolo (Katavi), Dk Athuman Kihamia (Arusha) na Hassan Rugwa (Dar es Salaam).

Wengine ni Dk Fatuma Mganga (Dodoma), Musa Chogero (Geita), Mwanasha Tumbo (Pwani), Prisca Kayombo (Simuyu) na Pili Mnyema (Tanga).

Join our Newsletter