Uko hapa: NyumbaniHabari2021 05 29Article 540460

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia aahidi jitihada kufikia 50/50 katika uongozi

Samia aahidi jitihada kufikia 50/50 katika uongozi Samia aahidi jitihada kufikia 50/50 katika uongozi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha anaongeza jitihada za kufikia usawa wa kijinsia wa nusu kwa nusu (50/50) katika uongozi.

Aidha, imebainika kuwa Rais Samia amekubali kuwa kiongozi katika eneo la haki za kiuchumi katika mkutano utakaojadili masuala ya kijinsia uliopangwa kufanyika Juni 30, mwaka huu jijini Paris nchini Ufaransa.

Hayo yamebainika Ikulu, Dar es Salaam jana wakati Rais Samia alipokutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN-Women), Dk Phumzile Mlambo-Ngcuka kuhusu kuendeleza ajenda zinazowahusu wanawake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Samia ameipongeza UN-Women kwa juhudi kubwa za kupigania masuala ya wanawake ikiwemo maazimio ya Beijing.

Alieleza Tanzania ipo tayari kuungana na UN-Women katika kuongeza msukumo wa utekelezaji wa maazimio hayo.

Rais Samia alibainisha kuwa japo Tanzania bado haijafikia kiwango cha usawa wa kijinsia cha 50/50 katika uongozi, katika kipindi chake atahakikisha anaongeza jitihada za kufikia usawa huo.

Aliishukuru UN-Women kwa utayari wake wa kuisaidia Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Naye Dk Mlambo-Ngucka alimshukuru Rais Samia kwa namna anavyounga mkono juhudi za kupigania masuala ya wanawake na ameahidi kuwa UN-Women itamuunga mkono katika juhudi hizo.

Alimualika kushiriki katika mkutano utakaojadili masuala ya kijinsia uliopangwa kufanyika Juni 30, mwaka huu Paris, Ufaransa ambao madhumuni yake ni kuchagiza usawa wa kijinsia kama yalivyokubaliwa katika mkutano wa Beijing uliofanyika mwaka 1995 baada ya kuonekana baadhi ya maazimio yanasuasua.

“Kuelekea mkutano huo nchi zitakazoshiriki zimegawanywa katika maeneo sita ya kufanyia kazi na Mheshimiwa Rais Samia amekubali kuwa kiongozi katika eneo la haki za kiuchumi,” ilieleza taarifa ya Ikulu.

Aidha, Dk Mlambo-Ngcuka alieleza kufurahishwa kwake na sekta binafsi ya Tanzania ambayo imekubali kushirikiana na serikali kusaidia juhudi za kuleta usawa wa kijinsia katika masuala ya kiuchumi kwa wanawake.

Join our Newsletter