Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541855

Habari Kuu of Wednesday, 9 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia aanika mikakati kuinua wanawake

Samia aanika mikakati kuinua wanawake Samia aanika mikakati kuinua wanawake

RAIS Samia Suluhu Hassan ameainisha mikakati mbalimbali ya kuwasaidia wanawake kuinuka kiuchumi ikiwemo kutumia mifuko 61 ya kuwawezesha wanawake kiuchumi iliyoundwa tangu Uhuru ambayo mpaka sasa imetoa jumla ya Sh trilioni 2.2 kwa wanawake.

Akizungumza kwenye mkutano wake na wanawake zaiid ya 14,000 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Raos Samia alisema kuhusu uwezeshaji wanawake kiuchumi, jitihada kubwa zimefanyika kutokana na serikali kuanzisha jumla ya mifuko 61 kwa lengo hilo.

“Mifuko hii mingine imekuwa kiishia kati kati na kuundwa mingine mpaka tulipofika, na leo nina furaha kumuona mdogo wangu Beng’i Issa (Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi) yupo hapa, kwenye mfuko wa kuwezesha wanawake kiuchumi tulimpa dhamana ya kuingalia mifuko mingine yote ili atuambie mfuko gani una uhai uendelee na mfuko gani hauna uhai tuachane nao,” alisema Rais Samia.

Milioni 5.3 wafaidika

Alisema wanawake waliofaidika na mikopo iliyotolewa na mifuko hiyo ni milioni 5.3. Aliwataka kujitathmini fedha hizo zimefanya nini, wamepata mafanikio gani, lakini pia kutathmini kama kweli fedha zote ziliingia mikononi mwa wanawake, hivyo wana kazi ya kutathmini jitihada za serikali na mavuno ambayo wamevuna kwa sasa.

“Mwaka 2018 serikali ilipitisha sheria iliyozielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo isiyo riba kwa wanawake asilimia nne, vijana asilimia nne na wenye ulemavu asilimia mbili,” aliongeza.

Alisema tangu kipindi hicho, mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 63 ilitolewa na kuwanufaisha wanawake zaidi ya laki tisa, pia Benki ya Posta Tanzania kupitia dirisha la wanawake imeendelea kutoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 22.3 kwa wanawake 6,327.

Aonya madiwani

Kutokana na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri, alisema kwa muda mrefu baadhi ya madiwani wametumia mfuko huo kujijenga kisiasa kwa kutoa kiasi kidogo cha Sh milioni 1.5 kwa kikundi chenye watu kati ya wanane hadi tisa.

“Ukiangalia hali ya uchumi, milioni 1.5 kwa watu tisa wanakwenda kufanya kazi gani, ndiyo maana fedha hizi mzunguko wake ukawa mdogo, mikopo hii hairudi kwa sababu wananchi wanaoipokea iwe wanawake, vijana au walemavu, wanahisi ni hisani kutoka kwa madiwani wao, kwa hiyo mikopo hairudi,” alisema Rais Samia.

Aliongeza, “Kwa sababu ukiangalia fedha hizi na fedha walizotoa Benki ya Posta Sh bilioni 22 kwa wanawake 6,300, unaona kabisa hapa kuna fedha ya maana imetoka na pengine kuna mambo ya maana yangefanyika.”

Kutokana na changamoto hiyo ya mikopo ya halmashauri, Rais Samia alimwagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu kusimamie vikundi vyenye sida ili vipate mikopo bila ubaguzi kwa kuwa kuna tuhuma za mikopo kutolewa kwa upendeleo.

Alisema mwaka 2016 wakati akiwa Makamu wa Rais, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alimteua kuwa mjumbe wa jopo la dunia katika kumwezesha mwanamke kiuchumi katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika chini ya Jangwa la Sahara.

“Lengo kuu la jopo hilo lilikuwa kuandaa mikakati thabiti ya kitaaluma na iliyohakikiwa katika kuziba pengo kati ya wanawake na wanaume duniani kupitia mkakati wa kumwezesha mwanamke kiuchumi. Pi kuifanya ajenda ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kuwa ajenda ya kidunia ili kufikia malengo endelevu ya kufikia usawa wa kijinsia na hasa lengo la tano ya malengo ya kidunia,” alisema Rais Samia.

Majukwaa ya uwezeshaji

Alisema katika kutimiza majukumu yake kwenye kazi hiyo, kwa nchini alibuni wazo la kuanzisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa lengo la kuwakutanisha wanawake ili kujadili fursa, changamoto na jinsi ya kushiriki kikamilifu katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

Alisema kwa wakati ule jumla ya majukwaa 23 yaliundwa katika ngazi ya mikoa na kuongeza kuwa anafarijika kuona mpaka sasa majukwaa 18 kwa takwimu bado yapo na yanaendelea kufanya kazi, pia majukwaa 144 yaliundwa katika ngazi za halmashauri za wilaya, majukwaa 302 ngazi ya kata na majukwaa 522 katika ngazi ya kijiji au mtaa.

“Nitumie fursa hii kuiagiza mikoa, wilaya na halmashauri kuendelea kuyatunza na kuyasimamia majukwaa haya. Nalisisitiza hivyo kwa sababu sasa najipanga kikamilifu kuyalea majukwaa haya. Ndani ya Ofisi ya Rais kulikuwa na mfuko wa kujitegemea, nimepekua makabrasha nikakuta hiki kipengele, nikasema nitatumia mfuko huu huu kulea majukwaa,” alisisitiza Rais Samia.

Alisema kwa taarifa zilizopo, ni asilimia 7.4 pekee ya wanawake ndiyo wanaumiliki wa nyumba ya peke yao ikilinganishwa na silimia 25.6 ya wanaume, pia wanawake wanaomiliki ardhi peke yao ni asilimia 8.1 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia kubwa.

Pia alisema wakati wa mkutano wa Afrika na Ufaransa uliofanyika hivi karibuni ambao alishiriki kwa njia ya video, alipewa heshima ya kuchagua eneo moja la kumjenga mwanamke ili Tanzania ilisimamie.

Alisema katika mkutano huo aliamua kuchagua eneo la haki za kiuchumi kwa wanawake kwa kutambua kuwa uwezeshaji wanawake kiuchumi ni nguzo muhimu ya kuleta usawa wa kijinsia.

“Naju kati yetu hapa kuna vijana wazuri katika mabenki akiwemo ndugu yetu wa Benki ya NMB, Ruth (Zaipuna) na wanawake wote waliopo kwenye sekta za kiuchumi watanisaidia kufanyna uchambuzi wa hali halisi ilivyo ndani ya Afrika na ndani ya nchi yetu ili kuona maeneo gani yana mapengo, maeneo gani tungependa tusaidiwe nini, na tunataka kwenda mpaka wapi ili tukayawasilishe katika kuisaidia Afrika katika eneo la haki za wanawake kiuchumi,” alisema Samia.

Rais Samia pia aliwataka wanawake wote kumuunga mkono na kumsaidia katika ujenzi wa Tanzania na kulifikisha Taifa hili linapostahili kuwa.

Join our Newsletter