Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 26Article 544276

Habari Kuu of Saturday, 26 June 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia ahadharisha wimbi la 3 la corona

Samia ahadharisha wimbi la 3 la corona Samia ahadharisha wimbi la 3 la corona

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaomba viongozi wa dini na Watanzania wote kurejea kwa Mwenyezi Mungu kumuomba anusuru taifa dhidi ya Covid- 19 kwa kuwa wimbi la tatu la ugonjwa huo lipo nchini.

Samia ambaye amewataka maaskofu wa Kanisa Katoliki kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo, amesema tayari nchini wapo wagonjwa wa Covid-19 kama alivyoelezwa alipotembelea Hospitali ya Manispaa ya Kinondoni ya Mwananyamala, Dar es Salaam hivi karibuni na kuoneshwa wodi walikolazwa.

Alisema hayo leo alipozungumza katika mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ulioshirikisha viongozi wa taasisi, jumuiya na mashirika yaliyo chini ya kanisa hilo nchini.

Mkutano huo ulifanyika katika Ukumbi wa TEC, Kurasini, Dar es Salaam.

“Dunia ina janga hili, kanisa tangu mwanzo limekuwa thabiti kupambana na ugonjwa huu… niwaombe maaskofu, pamoja na mambo mengine msisahau kuwakumbusha waumini umuhimu wa kujilinda na kuchukua tahadhari dhidi ya corona,” alisema Samia.

“Tusiache kutumia kila kitakachotulinda na maradhi haya. Duniani sasa kuna wimbi la tatu. La kwanza Tanzania tumeingia, la pili tumeenda nalo sasa kuna la tatu, ishara inaonekana, tuna wagonjwa wameonekana wakiwa na tatizo hili.”

Aliongeza; “Mwananyamala kuna wodi ya Covid-19. Hili jambo bado lipo niwaombe viongozi wa dini mliseme hili kwa sauti kubwa ili tuepukane na janga hili. Tumuombe Mungu kwa nguvu zote yeye ndiye muweza wa yote.”

Rais Samia alinukuu vifungu vya Biblia Takatifu katika Zaburi 91:4 na Yeremia 33:6 vinavyoeleza ukuu wa Mungu katika kuwalinda watu wake kwa kuwafunika kwa mbawa zake na kuwapa hifadhi na ulinzi na kushusha afya na uponyaji, wastarehe kwa amani na utulivu.

Alisema pamoja na njia zote za sayansi, Watanzania hawana budi kumrejea Mungu kumuomba kwa dhati juu ya janga hilo.

Akitoa neno la shukrani, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadei Ruwa’ichi alimshukuru Rais kwa kutambua mchango wa kanisa katika ustawi wa taifa na kumuahidi kumuunga mkono katika yote ikiwamo vita dhidi ya corona.

Askofu Ruwa’ichi alimshukuru kwa heshima aliyompa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo hilo, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo kwa kumpa cheti cha shukrani na fedha za ujenzi wa kanisa katika Ibada ya Misa Takatifu ya maadhimisho ya miaka 50 ya upadri iliyofanyika Juni 20, mwaka huu, Dar es Saalaam.

“Sisi raia wako na washiriki wa kusukuma gurudunmu la maendeleo tunakuahidi ushirikiano wa dhati kudumisha haki, amani, umoja na mshikamano wa taifa. Tunakuadihi kukuweka katika sala zetu ili Mungu akusaidie na kukuongoza kuliongoza taifa. Mungu akudumishe katika afya njema na uthabiti wa jukumu la kuliongoza taifa,” alisema Ruwa’ichi.