Uko hapa: NyumbaniHabari2021 06 09Article 541852

Habari Kuu ya

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia asisitiza miradi yote kukamilika 2025

Samia asisitiza miradi yote kukamilika 2025 Samia asisitiza miradi yote kukamilika 2025

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ifikapo mwaka 2025 serikali itakuwa imekamilisha miradi yote iliyoanza kutekelezwa katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Akizungumza na wanawake zaidi ya 14,000 mkoani Dodoma jana, Rais Samia alisema mkakati wa serikali yake ni kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano inakamilika ifikapo 2025.

Rais Samia alisema ni kweli kilio kikubwa na maswali mengi bungeni ni kuhusu suala la maji, na kwamba wakati mwingine Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi anajibu maswali hata yanayomzidi kimo wakati yeye ni mfupi.

Hata hivyo, alisema mbio kwenda maeneo ya maji kuhakikisha maji yanapatikana zinaonekana, yeye Naibu Waziri Mahundi akimaliza kujibu maswali anakwenda upande wake na Waziri Jumaa Aweso anakwenda upande wake.

“Kufika 2025 tutakuwa tumekamilisha kama tuliyoagizwa na Ilani ya CCM 2020-2015 kupeleka maji miji na kwenye majiji asilimia 95 na kwenye vijiji asilimia 85 tutakamilisha au hata kuzidi kudogo. Lengo ni kumtua ndoo mama kichwani,” alisema Rais Samia katika mkutano huo mkubwa na wanawake nchini.

Rais Samia alisema upatikanaji maji safi na salama kuanzia Uhuru hadi kuingia awamu tano mwaka 2015, umewezesha kupeleka maji kwa Watanzania asilimia 74, sasa imebaki asilimia 26 tu kupatiwa huduma hiyo.

Kuhusu umeme hasa vijijini, alisema, “tunakwenda kumaliza vijiji vilivyobaki 2,024, vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme. Usambazaji utabaki, tunafundisha mabwana umeme wengi vyuoni ili wasaidie kazi ya kusambaza umeme vijijini.”

“Wanawake wenzangu tunatakiwa kutumia umeme kwa ajili ya shughuli za kiuchumi, si kumulikia na kuona,” alisema.

Kuhusu sekta ya usafiri na usafirishaji, Rais Samia alisema ili kurahisisha usafirishaji watu na mizigo kupitia barabara, maji, anga, reli na awamu ya tano imefanya vizuri na Serikali ya Awamu ya Sita itafanya vizuri zaidi ili kumaliza ujenzi miundombinu iliyoanza na awamu ya tano.

Katika kukamilisha mradi hiyo inayohusu miundombinu aliutaja Uwanja wa Kimaita wa Ndege wa Msalato jijini Dodoma, na pia serikali inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambako Rais Samia wiki hii atakwenda Mwanza kuweka jiwe la msingi la loti ya tano ya reli hiyo. Pia loti ya tatu na nne zilizobaki zitakwenda kwa kasi ili kumaliza.

Katika ziara ya Mwanza, pia Rais Samia atazindua meli mbili zilizojengwa pamoja na chelezo za kutengeneza meli zinazojengwa nchini. Lengo kubwa la serikali ni kuhakikisha usafiri na usafirishaji unapewa mkazo mkubwa.

Rais Samia alisema mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita ni kuiwezesha Tarura ili kujenga barabara za vijijini. Alisema barabara hizo zinapojengwa umadhubuti wake unakuwa hafifu na mvua ikinyesha misimu miwili inabomoka.

Hivyo aliongeza kuwa serikali inaangalia teknolojia itakayofanya zidumu muda mrefu. Pia itaiwezesha Tarura kifedha na kutalaamu katika kujenga na kukamilisha barabara hizo muhimu kwa wakulima hasa wanawake ambao asilimia 70 wapo vijijini wanajishughulisha na kilimo.

Lengo la serikali na kuboresha barabara hizo ni kusogeza huduma bora za barabara kwa wanawake ambao ndio wanahenya, hivyo pia ndio wanapata adha kwa kushindiwa kuzifikia huduma bora za afya.

Katika afya, alisema serikali imefanya juhudi kubwa kwani imesogeza huduma za afya vijijini na sasa asilimia 80 ya watoto wanazalisha kwenye vituo. Pia imeifanya Tanzania ikuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika kutoa chanjo kwa watoto kwa asilimia 98, hivyo kusaidia kupunguza vifo vya watoto na akinamama.

Rais alitoa mfano wa watoto wachanga chini ya siku 28 kwamba vifo vimeshuka hadi kufikia watoto saba katika kila vizazi hai 1,000, ambako alisema miaka ya nyuma walikuwa wakitajwa mamia, sasa ni vifo saba tu.

Pia vifo vya watoto wa chini ya miaka mitano vimeshuka hadi watoto 50 katika kila vizazi hai 1,000, huku vifo vya wajawazito vikishuka hadi 321 katika kila wajawazito 1,000, hatua zilizoshusha vifo vya wanawake wanapojifungua.

Join our Newsletter