Uko hapa: NyumbaniHabari2021 07 18Article 547357

Habari Kuu of Sunday, 18 July 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia ataka vikwazo vya biashara Tanzania, Burundi viondolewe

Gharama ujenzi wa hospitali zamshtua kiongozi wa Mwenge Gharama ujenzi wa hospitali zamshtua kiongozi wa Mwenge

RAIS Samia Hassan Suluhu amemuagiza Waziri wa Biashara na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kuhakikisha anashughulikia kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi.

Pia amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa kuboresha huduma za usafiri wa reli ili kuongeza usafirshaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara wa Burundi na idadi ya mizigo inayosafirishwa kwenda nchi hiyo.

Alitoa maagizo hayo jana wakati akihutubia mkutano wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi jijini Bujumbura, Burundi. Rais Samia ambaye alikuwa nchini humo kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili, alimaliza ziara yake jana na kurejea nchini. Alisema kufanyika kwa kongamano hilo ni ishara ya kuimarika uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Burundi. Alisema takwimu zinaonesha kampuni 17 za nchini zimewekeza Burundi katika sekta ya ujenzi, fedha, afya, usafirishaji na madini, huku 18 za Burundi zikiwa zimewekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Alisema takwimu hizo zinaonyesha jinsi nchi hizo zinavyofanya biashara kwa usawa ingawa jitihada zaidi zinahitajika kuwekeza katika maeneo mengi ambayo hayajafanyiwa kazi. Aidha, Rais alisema ni lazima kutumia kikamilifu fursa za soko lililopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzalisha bidhaa zilizoongezewa thamani.

Vilevile, alitaka kutumika kikamilifu fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo kuchochea upatikanaji wa ajira kwa vijana ambapo alisema Tanzania ina fursa nyingi ambazo wafanyabishara wa sekta binafsi wanaweza kuzitumia.

Rais Samia alisema Tanzania ina takriban hekta milioni 44 za ardhi nzuri ambazo kati ya hizo, hekta milioni 10 hazijatumiwa kikamilifu, hivyo amewashauri wafanyabiashara hao kutumia fursa ya hali ya hewa nzuri iliyopo nchini kuwekeza katika kilimo. Alisema serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam, Kigoma, Kalema, Kasanga na Kabwe ili kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa.

Aliwataka wafanyabiashara wa Burundi kuendelea kutumia bandari za Tanzania kikamilifu. Alisema eneo lingine ambalo Burundi inaweza kulitumia ni huduma ya afya ambayo Tanzania imewekeza kwa kiwango kikubwa kwa kuwa na wataalamu mahiri na vifaa vya kisasa, hususani vya matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo jijini Dar es Salaam na kuwaomba wananchi wa Burundi kuja nchini kupata huduma hizo.

Wakati huohuo, Rais Samia alikutakana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Burundi (Jutabu) na kuwashukuru kwa mapokezi mazuri tangu alipowasili nchini humo.

Alipoingza jumuiya hiyo kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii Burundi na Tanzania. Jutabu ilitoa mchango wa madawati na kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mwaka 2016 na pia wakati wa kuzama kwa meli ya MV Nyerere mwaka 2018.

Rais Samia aliwaeleza Watanzania hao hali ni shwari nchini na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida. Alisema raia wanaoishi nje ya nchi ni kundi muhimu kutokana na mchango wao kwa nchi zao kama walivyo wao wanaoishi Burundi. Inakadiriwa kuwa, Watanzania wapatao milioni moja wanaishi katika nchi mbalimbali duniani.

Samia alisema kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, Diaspora wa Tanzania mwaka 2018 walituma nchini dola za Marekani milioni 475.65. Alisema kutokana na umuhimu wao huo ndio maana serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania waishio nje ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Alitoa mwito kwa Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi kujiandikisha kwenye Balozi za Tanzania katika mataifa wanayoishi iwe rahisi kwa serikali kuwahudumia pamoja na kunufaika na fursa zinazopatikana nyumbani na kuwataka kujiepusha na vitendo vya uhalifu kwani vinachafua jina la Tanzania.