Uko hapa: NyumbaniHabari2021 10 23Article 565159

Habari Kuu of Saturday, 23 October 2021

Chanzo: www.habarileo.co.tz

Samia atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 10

Samia atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 10 Samia atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 10

WANANCHI wa jamii ya wafugaji kutoka Kijiji cha Kimotorock, Kata ya Loboisiret wilayani Simanjiro, wameeleza kufurahishwa na uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwarejeshea ardhi yao iliyotwaliwa na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa zaidi ya miaka 10.

Rais Samia kupitia kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza kurejesha kwa wananchi eneo lenye ukubwa wa ekari 4,392.7 lililokuwa likidhibitiwa na Hifadhi ya Tarangire na kuzua mgogoro baina yao na wakazi wa Kijiji cha Kimotorock.

Kiongozi wa kimila, Laigwanan Danieli ole Melau ambaye pia ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), tawi la Kimotorock alisema Rais Samia amekiheshimisha chama hicho kwa jamii ya wafugaji si tu wa kijiji hicho bali kwa wilaya nzima ya Simanjiro kwa uamuzi huo.

“Mgogoro huu umetutesa kwa muda mrefu ….Tunamshukuru sana Rais Samia kwa miezi sita tu aliyokaa madarakani amemaliza mgogoro huu,” alisema Melau.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mtendaji wa Kijiji cha Kimotorock, Pateli Kivuyo alisema uamuzi wa rais umekuwa faraja si tu kwa wananchi bali hata kwa watendaji wa serikali kijijini hapo na vitongoji vyake.

“Tulikuwa tunapata shida sana kusimamia baadhi ya shughuli nyingine za maendeleo kutokana na mgogoro huo wa ardhi baina ya kijiji na Hifadhi ya Tarangire kwa upande mmoja na Pori la Mkungunero kwa upande mwingine kutokana na wananchi kuona sisi wote watumishi wa serikali tunawanyanyasa,” alisema.

Uamuzi huo wa Rais Samia uliwasilishwa rasmi katika kijiji hicho wiki iliyopita na Waziri Lukuvi akiwa ameambatana na mawaziri wengine saba. Alisema utekelezaji huo umeanza siku hiyo ya tamko.

Mgogoro wa kijiji hicho na pori la hifadhi ya Mkungunero uliodumu kwa miaka zaidi 10 licha ya kuhusisha kijiji hicho lakini pia unahusisha Mkoa wa Manyara na Dodoma kutokana na pori hilo kutambulika lipo katika Wilaya ya Kondoa, mkoani Dodoma.