Uko hapa: NyumbaniHabari2022 01 11Article 584926

Habari Kuu of Tuesday, 11 January 2022

Chanzo: www.tanzaniaweb.com

Samia avipa 'homework' vyuo vya ufundi nchini

Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan amevitaka vyuo vya mafunzo ya amali na vinavyofundisha ushonaji vifundishe kwa bidii ili kuzalisha watu wenye sifa ya kuajiriwa.

Ameyasema hayo leo Januari 11, 2022 wakati akizindua kiwanda cha nguo cha Basra Textile Mills, Chumbuni Zanzibar ikiwa ni sehemu ya maonyesho ya kuelekea miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema uzoefu unaonyesha kwamba nchi nyingi za Asia kwamba wanaoajiriwa sana kwenye viwanda vya nguo ni wanawake.

“Hii ni kwasababu wanawake ni watulivu na waangalifu sana. Kwasababu unaposhona nguo ya kimataifa haitaki papara, inataka utulie ufikie vigezo vinavyohitajika na pia mikono yao ni laini kuweka vifungo, kutunga sindano na vitu vingine.

“Lakini fikirieni mikono ya mwanaume ishike vifungo! Kwahiyo hapa ni fursa ya ajira kwa wanawake wengi. Kinamama kasomeni ushoneni fursa iko hapa,” amesema Rais Samia.

Amesema matarajio ni kwamba siku za usoni kuacha kuagiza bidhaa hizo kutoka nje hasa nguo za watoto pamoja na kusafirisha kwenda soko la ukanda wa Afrika Mashariki na baadae eneo la ukanda wa SADC.

“Kwahiyo hii ni fursa nzuri kwetu kutumia masoko mawili kupeleka bidhaa zetu huko. Muione fursa hii ili katika kipindi hiki ambapo muwekezaji anajiandaa kuwekeza phase ya pili tuwe tumeshajiandaa,” amesema.